Wazazi wote Wilayani Newala, wameaswa kuutambua umuhimu wa Elimu kwa watoto wao ukizingatia kuwa maisha ya sasa yanahitaji taifa lililo elimika zaidi kwa msingi wa maisha.
Wito huo umetolewa na kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Bwana Alford Mpanda katika sherehe za maadhimisho ya juma la Elimu kiwilaya, yaliyofanyika jana tarehe 10/07/2018 katika shule ya msingi Kitangali Mazoezi Wilayani Newala.
Bwana Mpanda amesema kuwa, wazazi wana jukumu kubwa la kufualitila maendeleo ya watoto wao shuleni ili waweze kufanya vizuri, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanakuwa na tabia njema na nidhamu wakati wote, jambo litakalopelekea kuwasaidia walimu katika kuwafundisha na kuwalea vizuri wakati wote wa masomo yao.
Aidha wadau wote wa elimu pamoja na wazazi kwa ujumla wametakiwa kuhakikisha wanawafatilia pia watoto wenye mahitaji maalumu, ili nao waweze kupata haki yao ya msingi katika elimu, kwani kumekuwa na kawaida kwa baadhi ya wazazi kuwatenga na kuwaficha watoto walemavu, jambo linalopelekea kuwakosesha elimu na kujifunza mambo mbalimbali.
Kwa upande wa kitengo cha elimu maalum katika shule ya Kitangali Mazoezi, mkuu wa kitengo hicho Mwalimu Jafari Mnambe, amesema kazi kubwa wanayoifanya kwa sasa, ni kuwabaini watoto wenye mahitaji maalum katika vijiji vyote vya Tarafa ya Kitangali, kuwasajili shule na kuwabadilisha tabia zao za nyumbani, ili wajifunze maisha ya shule ambayo ni ya kimtaala wa elimu ya msingi.
Pamoja na changamoto za umbali na nyinginezo zikiwemo kukosekana kwa usafiri wa kutembelea shule mbalimbali, kitengo hicho cha elimu maalum, kiliweza kutembelea shule za kata nne za Maputi, Kitangali, Vihokoli na Nandwahi, ambapo katika ziara hiyo walifanikiwa kuwabaini watoto wenye mahitaji maalum ili wajiunge na wenzao waliopo katika kitengo cha elimu maalum kilichopo shule ya msingi Kitangali Mazoezi.
Baadhi ya wanafunzi wa shule mbalimbali za msingi na sekondari za Tarafa ya Kitangali wakionyesha mabango yenye ujumbe mbalimbali wa elimu wakati wa maandamano ya kilele cha maadhimisho ya juma la elimu, yaliyofanyika tarehe 10/07/2018 katika shule ya msingi Kitangali Mazoezi.
Kauli mbiu ya maadhimisho ya juma la elimu kwa mwaka huu wa 2018 ni “Stadi za KKK ni msingi wa elimu, tuwekeze katika elimu kwa uchumi wa viwanda”
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa