MAAFISA bajeti wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala wametakiwa kuhakikisha mipango na bajeti wanazoandaa zinaendana na mahitaji halisi ya wananchi, zinakuwa shirikishi, zinatekelezeka na zinazingatia uwazi pamoja na uwajibikaji katika hatua zote za maandalizi.
Wito huo umetolewa jana na Afisa Mipango wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala, Ndugu Sylvester Ngonyani, wakati akifungua mafunzo ya Uandaji wa Mipango na Bajeti kwa Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa, yaliyofanyika katika ukumbi wa Halmashauri hiyo.
Mafunzo hayo ni maandalizi ya bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027, ambapo utaratibu huu hufanyika kila mwaka kwa lengo la kuongeza ufanisi katika maandalizi na utekelezaji wa bajeti zinazogusa mahitaji ya wananchi. Ngonyani alisisitiza umuhimu wa kushirikisha ngazi zote katika michakato ya upangaji bajeti ili kuhakikisha mipango inayoandaliwa inatekelezeka kwa uhalisia.
Kwa upande wake, Afisa Bajeti (Mwezeshaji )wa mafunzo hayo kutoka Idara ya Mipango, Ndugu Aza Macha, aliwasilisha mada kuhusu Uandaji wa Mipango na Bajeti katika Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa, akisisitiza umuhimu wa kuwa na mipango yenye sifa za SMART—yaani mahsusi, inapimika, halisi, yenye muda maalum na inayotekelezeka.
Aidha, Ndugu Andrew Nyumayo, SN. DHRO, ambaye ni miongoni mwa washiriki wa mafunzo hayo, alielezea kufurahishwa na mafunzo hayo na kuahidi kuyafanyia kazi kikamilifu. “Tumejifunza mambo muhimu sana, nitahakikisha tunazingatia ushirikishwaji wa watumishi wote katika kila idara na kitengo wakati wa maandalizi ya bajeti,” alisema Nyumayo.
Mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya TAMISEMI yaliyopo kwenye Muongozo wa Uandaji wa Mipango na Bajeti, yakiwa na lengo la kuimarisha utendaji wa Serikali za Mitaa katika kusimamia rasilimali za umma kwa tija na maendeleo endelevu ya wananchi.
@ortamisemi
@mtwarars_habari
@msemajimkuuwaserikali
@newalafmtz
@chikaladigitaltv
@kizurdigital
Kitangari,Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa