Mkuu wa Wilaya ya Newala Mhe. Aziza Mangosongo leo tarehe 12/11/2019 amefanya kikao kazi na watendaji wa vijiji, watendaji wa kata, viongozi wa vyama vya msingi vya ushirika (AMCOS), meneja wa chama kikuu cha ushirika cha Tandahimba na Newala (TANECU), Afisa Ushirika, muwakilishi wa meneja wa NMB na meneja masoko wa Tigo kwa lengo la kujadili uendeshaji wa zoezi la uuzaji wa korosho na ulipaji wa wakulima kwa wakati.
Akizungumza na wajumbe wa kikao hicho, Mhe. Mangozongo amewataka kuhakikisha kilo zinazopimwa kwenye maghala ya AMCOS zinafika kwa usahihi katika maghala makuu; fomu zinajazwa vizuri kulingana na mzigo uliosafirishwa; kuwa na kituo kimoja cha malipo ambacho ni TANECU; magunia yanayotolewa na TANECU kuwekea korosho yahifadhiwe kwenye maghala ya AMCOS na si nyumbani; ubora wa korosho upimwe vizuri; wakulima ambao hawana namba za akaunti au tigo pesa korosho zao zisipokelewe; wakulima kutunza namba za siri za akaunti zao za benki au tigo pesa na Watendaji wa kata kutembelea maghala ya AMCOS kukagua ubora wa korosho, vitabu vya risiti na kujua idadi ya wakulima wanaodai katika kata husika.
Pia meneja wa TANECU Bw. Mohamed Nasoro alitumia kikao hicho kuwaeleza wajumbe kuwa TANECU wamejiandaa vizuri na msimu huu mpya wa korosho na kueleza tozo zilizopitishwa na wadau katika malipo ya kila kilo moja ya korosho ambayo ni Tsh.56.52 kwa ajili ya Halmashauri, Tsh. 25 kwa ajili ya bodi ya korosho, Tsh. 24 kwa ajili ya taasisi ya utafiti wa kilimo Naliendele, Tsh. 25 kwa ajili ya ushirika (AMCOS na TANECU). Jumla ya makato yote yatakayofanywa kwa mkulima katika kila kilo moja ni Tsh. 176.52 ukiondoa gharama za usafirishaji kutoka katika maghala ya AMCOS kwenda kwenye maghala makuu.
Wajumbe wa kikao hicho walijulishwa na meneja wa TANECU kuwa korosho za wilaya ya Newala zilizouzwa kwa mnada wa kwanza zilikuwa na thamani ya shilingi bilioni tisa na milioni arobaini na tisa ambapo baada ya makato jumla ya shilingi bilioni nane na milioni mia tano na tatu zimeshahamishwa kwenye akaunti za AMCOS kwa ajili ya malipo ya wakulima ambayo yameshaanza kufanyika. Mnada wa pili ulihusisha korosho zenye thamani ya shilingi bilioni tisa na milioni mia tano na sitini na mbili. Aidha mnada wa tatu unatarajiwa kufanyika siku ya Ijumaa tarehe 15/11/2019 katika eneo la Kitangari, Halmashauri ya Wilaya ya Newala.
Mhe. Mangosongo pia amewataka wananchi kutokujihusisha na biashara ya kangomba kwa kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa juu yao.
Kikao hicho ni moja ya mkakati wa Mhe. Mangosongo kuhakikisha wakulima wanalipwa kwa wakati.
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa