Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Gelasius Gasper Byakanwa alipofanya ziara ya kikazi katika Wilaya ya Newala siku ya Jumatano tarehe 29/01/2020.
Katika ziara hiyo Mhe. Byakanwa amekemea wazazi wasiowapeleka watoto shule na kuagiza watoto wote wanaotakiwa kuripoti shuleni waripoti haraka. Akisisitiza jambo hilo, Mhe. Byakanwa katika kijiji cha Nanda, kata ya Muungano, Halmashauri ya Wilaya ya Newala wazazi waliobainika kutokuwapeleka watoto shule walikamatwa na kupelekwa mahakamani ili kulipa faini kwa kutotekeleza wajibu wao wa kuwapeleka watoto shule.
Akiendelea na ziara hiyo, Mhe. Byakanwa pia amewaagiza Maafisa Tarafa na Watendaji wa Kata wote kuhakikisha vijana wanaoishi katika maeneo yao ya utawala wanafanya kazi na si kukaa vijiweni.
"Vijana wengi hawafanyi kazi, wanakaa vijiweni, kucheza pool table, kula na kulala wakiwategemea wazazi kuwafanyia kazi. Kuanzia leo nataka kila kijana aonyeshe shamba lake na shughuli anayofanya na kuna timu maalum itakuja kuhakiki " alisema Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Byakanwa.
Ziara hiyo pia ilihusisha kusuluhisha migogoro ya mipaka kati ya maeneo ya shule na mashamba ya wanakijiji ambapo Mhe. Byakanwa ameagiza mipaka yote ya shule kuainishwa na wanakijiji kutovamia maeneo ya shule kwa shughuli zozote zikiwemo za kilimo.
"Mkoa ninaouongoza mimi, ninataka uwe ni wa watu wanaopenda elimu, wachapa kazi na wanaojiletea maendeleo yao wenyewe", alisema Mhe. Byakanwa.
Ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Byakanwa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Newala ni ya kikazi na ilihusisha kukagua ujenzi wa vyumba vya madarasa, vyoo vya wanafunzi na walimu, mahudhurio ya wanafunzi shuleni na kuzungumza na wananchi ambapo shule za sekondari Makukwe na Mpotola, na shule za msingi Nanda na Mtunguru B zilitembelewa.
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa