Serikali imewaondoa viongozi wasiofaa wa vyama vya msingi vya Newala na Tandahimba katika utendaji wao kufuatia ubadhilifu na kukosa sifa za utendaji katika vyama vya msingi.
Hatua hiyo imefikia mara baada ya uchunguzi uliofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Gelasius Byakanwa na kamati yake ya ulinzi na usalama kwa Wilaya zote mbili za Newala na Tandahimba, na kubainisha rasmi katika mkutano maalum uliofanyika jana tarehe 25/07/2018 katika ghala la TANECU, uliohusha chama cha ushirika TANECU pamoja na viongozi wa vyama vyote vya msingi wa Newala na Tandahima.
Mhe. Byakanwa alisema kwa upande wa Tandahimba, wamewaondoa viongozi takriban 72 waliohusika na upotevu wa pesa za wakulima katika msimu wa mwaka 2017/2018 na kwamba chama kilichoongoza zaidi kwa upotevu wa pesa ni kile kilichopoteza milioni 176 mbali na vyama vingine ambavyo vimehusika kupoteza viwango tofauti tofauti, na kwa upande wa Newala viongozi 12 walioondolewa ni kutokana na kuwa na elimu ya darasa la saba kwa mujibu wa sheria, na viongozi sita nao wamehusika katika ubadhilifu.
Aidha viongozi wote waliohusika kwenye ubadhilifu na waliokosa elimu ya kidato cha nne lakini bado wapo kwenye ushirika wataondolewa, wenye elimu ya darasa la saba watakaobakia ni wale waliochaguliwa tu, na kwa watendaji wa kuajiriwa ni lazima wawe na elimu ya kuanzia kidato cha nne, lengo ni kuusafisha ushirika na kuufanya ushirika uwe na watu wanaojua majukumu yao na wanaoweza kusimamia maslahi ya wanachama wao na sio wale wanaoingia kwenye ushirika kwa malengo ya kujinufaisha wenyewe.
Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara amewataka wakulima wote wa Newala na Tandahimba kuhakikisha wanafungua akaunti zao binafsi kabla ya msimu wakorosho wa 2018/2019 kuanza, kwani jambo lililochangia kuchelewesha malipo ya wakulima katika msimu uliopita ni kutokana na wakulima wengi kukosa akaunti zao wenyewe na kuchelewa kufungua akaunti, hivyo kila mkulima ni lazima awe na akaunti yake kabla ya msimu kuanza na ambae hatakuwa na akaunti yake hatapata malipo.
Kufuatia hilo Mhe. Byakanwa amewaagiza makatibu na watendaji wote wa AMCOS kuhakikisha kabla ya msimu huu kuanza wanaorodhesha na kubandika majina ya wakulima wao au wataokauza korosho kwao, akaunti namba zao na benki zao ili uwe muongozo wa kuwatambua na kurahisisha mchakato wa malipo yao, na maafisa ushirika wasimamie hilo.
Msimu wa korosho wa mwaka 2018/2019 unatarajiwa kuwa na utofauti mkubwa utakaorahisisha mchakato wa malipo na kuleta tija kwa wakulima.
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa