Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Bw. Galasius Gasper Byakanwa amefanya ziara ya siku mbili kuanzia tarehe 18 mpaka 19 mwezi Januari 2018 katika Wilaya ya Newala kwa lengo la kujitambulisha kwa wananchi anaowaongoza.
Bw. Galasius Byakanwa akizungumza na watumishi wa wilaya ya Newala katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya wilaya ya Newala
Katika ziara yake, alizungumza na watumishi wa Newala, alishiriki kupanda miche ya korosho, kukagua ujenzi wa ofisi ya Halmashauri ya Mji Newala na kuzindua ugawaji wa pikipiki na guta kwa vikundi kupitia TAMOSA.
Akizungumza na wananchi wa Newala, Bw. Byakanwa amewataka kudumisha amani na utulivu miongoni mwao kwa kuwa ndiyo chimbuko kuu la maendeleo. Pia amewataka wananchi wa Newala kurudi kwenye misingi ya utanzania kwa kutambua wenyeji na wageni kwa kuanzisha daftari la makazi ambalo litasaidia kujua wakazi wa eneo husika kwa majina, maeneo wanayoishi na shughuli wanazofanya.
Bw. Byakanwa amesisitiza juu ya zoezi linaloendelea la uandikishaji na utoaji wa vitambulisho vya taifa, ambapo amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika zoezi hilo ili wapate vitambulisho hivyo kwa kuwa vitawasaidia katika mambo mbalimnbali yakiwemo kumtambulisha mtu kuwa ni mtanzania, kutumika kuomba pasi ya kusafiria ‘passport’ na kufungulia akaunti.
Pia amesisitiza kuzingatia mipangomiji kwa maafisa ardhi kuhakikisha wanatoa vibali vya ujenzi kabla ya zoezi la ujenzi kuanza na kupima maeneo na kuyatenga kwa kuzingatia matumizi bora ya ardhi.
Akiendelea kuzungumza, Bw. Byakanwa amewataka wananchi wa Newala kujiunga na mfuko wa afya ya jamii (CHF) kwa kuagiza walengwa wa kaya masikini wanaosaidiwa na Mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAF) kujiunga na CHF kwa kuchangia shilingi elfu kumi kwa kila kaya na wakatwe fedha hizo katika malipo yao.
Pia amewatoa hofu wakazi wa Newala juu ya swala la ukatikaji wa mara kwa mara wa umeme kwa kuwaeleza kuwa hali hiyo inasababishwa na uwezo mdogo wa uzalishaji wa umeme kwa mashine tulizonazo ambao ni megawatts 15.8 na kwa sasa utaratibu wa kuunganishwa kwenye gridi ya taifa unafanyika na pia zimeagizwa mashine mbili zitakazosaidia kuongeza uzalishaji wa umeme hadi kufikia megawatts 22.
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Bw. Byekanwa akizindua moja ya pikipiki ya vikundi vya vijana
Bw. Bakanwa pia ametumia ziara hiyo kukataza walimu kuchangisha michango kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari na kuwataka walimu kuusoma vizuri waraka wa elimu bure kwa kuwa ndio unaotuongoza kuzuia michango hiyo.
Pia ziara hiyo ilihusisha utembelewaji wa shamba la NEDECO lililopo katika kijiji cha Nanguruwe wilaya ya Newal, kukagua ujenzi wa ofisi mpya ya Halmashauri ya Mji wa Newala, kushiriki kupanda miche ya korosho katika kijiji cha Mtangalanga na kuzindua ugawaji wa pikipiki na guta kwa vikundi kupitia TAMOSA katika kijiji cha Chikunda Lubido.
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa