Mkuu wa Wilaya ya Newala Bi. Aziza Mangosongo amefanya kikao kazi na waratibu elimu kata pamoja na walimu wakuu wa shule za msingi na wakuu wa shule za sekondari za Wilaya ya Newala kwa siku mbili kuanzia tarehe 29 hadi 30 mwezi Julai, 2019.
Bi. Mangosongo ameitisha kikao hicho kwa lengo la kujadili maswala mbalimbali yanayohusu elimu na kupata mrejesho wa utekelezaji wa maagizo mbalimbali ya viongozi yakiwemo kumaliza ‘syllabus’ mapema ili kuwawezesha wanafunzi kufanya marudio na mitihani ya kujipima kwa wingi, kudhibiti utoro katika shule zetu, kubandika majina ya wanafunzi waliofanya vizuri kwenye mitihani ya Taifa katika mbao za matangazo za shule husika ili kuleta mori kwa wanafunzi wengine kufanya vizuri na uwepo wa bendera za Taifa katika shule zote za msingi na sekondari kwa kuwa hizo zote ni taasisi za Serikali.
Aidha, kikao hicho kilijadili pia maandalizi ya mitihani ijayo ya Taifa na Bi. Mangosongo amewataka walimu kuwapima wanafunzi kwa mitihani mbalimbali ya majaribio ili kujua uelewa wao na kufanyia kazi mada zote zinazoonekana kutoeleweka vizuri kwa wanafunzi wao.
Pia Bi. Mangosongo amewataka waratibu elimu kata kuwasaidia walimu wakuu katika kudhibiti utoro wa wanafunzi, kusimamia nidhamu kwa walimu na wanafunzi na kufuatilia na kusimamia miradiya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo ya shule ambayo imepatiwa fedha kutoka Serikalini. Aidha mafundi wote wanaopata kazi katika miradi hiyo lazima wawe na vitambulisho vya ujasiriamali vilivyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. John Pombe Joseph Magufuli.
Kikao hicho kilihitimishwa kwa walimu na waratibu elimu kata wote kuondoka na mikakati ya ufaulu ya kiwilaya ambayo ni kuwa na ushirikiano mkubwa baina ya walimu, kufanyika kwa vikao vya mara kwa mara vya walimu ili kujadili mafanikio na changamoto walizonazo katika utekelezaji wa majukumu yao na namna ya kutatua changamoto hizo, kufanyika kwa vikao vya kamati za shule, viongozi kutembelea kwenye shule mara kwa mara na kutoa ushauri, upatikanaji wa chakula shuleni ili wanafunzi wapate muda mwingi wa kujifunza, kuunda kwa kambi za wanafunzi kwa ngazi ya kata ili wanafunzi wabadilishane uzoefu na walimu washirikiane katika kufundisha na kumaliza ‘syllabus’ mapema.
Mikakati mingine iliyowekwa kwenye kikao hicho ni pamoja na kudhibiti utoro shuleni, kusimamia nidhamu kwa walimu na wanafunzi, kufanyika kwa mitihani ya kujipima ya mara kwa mara na utoaji wa zawadi kwa wanafunzi wanaofanya vizuri ili kuleta motisha kwa wanafunzi wengine kutamani kufanya vizuri zaidi.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Kaimu katibu Tawala wa Wilaya ya Newala Bw. Lincolin Tamba, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Bw. Mussa Chimae, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Newala Bw. Andrew Mgaya, Afisa Utumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Bi. Nancy Lyimo, Kamanda wa TAKUKURU wilaya ya Newala Bw. Bernad Mkama, maafisa idara ya elimu msingi na sekondari, waratibu elimu kata, walimu wakuu wa shule za msingi na wakuu wa shule za sekondari zilizopo katika wilaya ya Newala.
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa