Bodi ya mfuko wa Elimu Wilayani Newala imeridhika na kufurahishwa na jitihada kubwa za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Elimu inayotekelezwa na Halmashauri ya Wilaya ya Newala kupitia mfuko wa Elimu.
Akizungumza mara baada ya ziara ya kutembelea miradi ya mfuko wa Elimu iliyofanyika tarehe 18/06/2018 katika shule za vijiji na kata tofauti tofauti Wilayani Newala, Mwenyekiti wa Bodi ya mfuko wa Elimu ya Halmshauri ya Wilaya ya Newala Mzee Mohamedi Abeid Liyanga, amesema bodi yake imeridhika na kufurahishwa na jitihada za hali ya juu za viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala katika kuhakikisha wanatekeleza ipasavyo miradi ya mfuko wa Elimu, ili iweze kusaidia kuboresha swala zima la Elimu bora kwa watoto waliodhamiria kusoma kwa bidii waweze kufaulu na kusonga mbele zaidi, na kwamba changamoto za kielimu zilizokuwa zinatokana na mapungufu ya baadhi ya miundombinu na kukosekana kwa huduma za msingi katika baadhi ya shule, zitakuwa zimetatuliwa.
Mzee Liyanga ameongeza kuwa, utekelezaji wa miradi hiyo unaonyesha dhahiri kuwa fedha za mfuko wa Elimu zilizotumika mpaka sasa, zinawiana vizuri na hali halisi ya hatua ya miradi ilipofikia, na hii inamaanisha kuwa ubora wa miradi hiyo umezingatia thamani ya pesa zilizokusudiwa.
Wakati huo huo Mwenyekiti wa bodi hiyo amewashukuru wazazi na wananchi wa Newala hususani wale wa maeneo ya miradi husika, kwa kushirikiana vyema na serikali katika kuongeza nguvu ya utekelezaji wa miradi ya Elimu, ambayo ndiyo dira ya watoto katika Elimu na maisha yao ya baadae, amewaasa wazidi kuendelea kujitolea kushiriki katika ujenzi na uboreshaji wa shule mbalimbali ili kuinua kiwango cha Elimu Wilayani Newala.
Awali shule mbalimbali za msingi na sekondari Wilayani Newala, zilionekana kukosa baadhi ya huduma za msingi kama vyoo na upungufu wa vyumba vya madarasa, jambo lililowaathiri wanafunzi wengi katika maendeleo ya taaluma na afya bora.
Ziara hiyo iliyowahusisha wajumbe wa bodi ya mfuko wa Elimu ya Halmashauri ya Wilaya ya Newala akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Newala Mhe. Aziza Mangosongo, walifanikiwa kutembelea miradi mbalimbali ya Elimu ikiwemo ukarabati wa vyumba viwili vya madarasa shule ya sekondari Ushirika iliyopo Kata ya Mkwedu uliogharimu jumla ya shilingi milioni 7 mpaka sasa, mradi wa vyumba vitano (5) vya madarasa shule ya sekondari Makukwe ambao hadi kukamilika utagharimu shilingi milioni 80 na laki sita (80,600,000/=) ambazo zinatokana na michango ya wananchi kwenye mfuko wa Elimu kupitia makato ya mauzo ya zao la korosho, ukaguzi wa ujenzi wa vyoo matundu manne shule ya msingi Mbuyuni iliyopo Kata ya Makukwe unaogharimu shilingi 2,518,000/= zilizotolewa na mfuko wa Elimu, mradi wa vyumba viwili (2) vya madarasa shule ya sekondari Vihokoli unaogharimu jumla ya shilingi milioni 30 laki 2 na elfu hamsini (30,250,000) ambapo kiasi ch shilingi 250,000/= ni michango ya wananchi wa Vihokoli, miradi mingine ni ujenzi wa vyoo matundu 6 na madarasa 2 shule ya sekondari Lengo,na umaliziaji wa ujenzi wa matundu 4 ya vyoo shule ya Msingi Lengo na umaliziaji wa ujenzi wa madarasa 2 na matundu 8 ya vyoo shule ya sekondari Malatu.
Mwenyekiti wa bodi ya mfuko wa Elimu Mzee Mohamedi Abeid Liyanga (aliyenyoosha mkono) akiwa pamoja na wajumbe wa bodi wakikagua ujenzi wa vyoo matundu 4 shule ya Msingi Mbuyuni iliyopo Kata ya Mkukwe tarehe 18/06/2018.
Wajumbe wa bodi ya mfuko wa Elimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala wakikagua mradi wa ujenzi wa vyumba 2 vya madarasa ya shule ya Sekondari Vihokoli Tarehe 18/06/2018.
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa