Maafisa waandikishaji wasaidizi katika ngazi ya kata kwa Halmashauri ya Wilaya ya Newala leo tarehe 05/01/2020 wamepatiwa mafunzo maalum juu ya wajibu wao na taratibu za kufuata kwenye zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura.
Katika mafunzo hayo, maafisa waandikishaji ngazi ya kata pia walipata nafasi ya kujifunza kwa vitendo namna ya kujaza fomu zote zitakazotumika katika zoezi la uandikishaji na kutumia ‘BVR kit’ kuwaandikisha wapiga kura wapya, kubadili taarifa za wapiga kura wanaofanya mabadiliko na kuwaondoa wapiga kura ambao wamekosa sifa kwa sababu mbalimbali ikiwemo kifo.
Akifungua mafunzo hayo, Afisa mwandikishaji wa Jimbo la Newala Vijijini Bw. Mussa Chimae amewataka maafisa waandikishaji wasaidizi ngazi ya kata kuzingatia maelekezo watakayopewa katika mafunzo hayo.
“…..mawakala wa vyama vya siasa wataruhusiwa kuwepo katika vituo vya kuandikisha wapiga kura, jambo hili ni muhimu kwani linasaidia kuleta uwazi katika zoezi zima ila ieleweke kuwa hawatakiwi kuwaingilia watendaji wakati wanatekeleza majukumu yao.” Alisema Bw. Chimae.
Bw. Chimae pia aliwataka waandikishaji wasaidizi ngazi ya kata kuhakikisha wanavitunza vifaa vyote vitakavyotumika katika zoezi la uandikishaji wa wapiga kura kwani vimenunuliwa kwa gharama kubwa sana.
Mafunzo hayo ya siku moja yamefanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya kijiji cha Kitangari na yametolewa na maafisa waandikishaji wasaidizi ngazi ya jimbo la Newala Vijijini wakishirikiana na maafisa waandikishaji ngazi ya tume ya Uchaguzi ambapo maafisa waandikishaji ngazi ya kata wanatakiwa kwenda kutoa mafunzo hayo kwa waendeshaji wa mashine hizo na waandishi wasaidizi watakaohusika na uandikishaji wa wapiga kura katika vituo vya kuandikishia wapiga kura.
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa