Mwenyekiti wa Umoja wa wanawake (UWT) wa mkoa wa Mtwara Bi. Zuhura Farid jana tarehe 08/03/2020 amewaongoza wakazi wa Newala katika kuadhimisha siku ya wanawake duniani.
Maadhimisho hayo yalifanyika kiwilaya kwa wakina mama kushiriki katika shughuli za awali za ujenzi wa zahanati katika kijiji cha Nanguruwe kilichopo katika kata ya Nanguruwe Halmashauri ya mji wa Newala.
Pia wanawake wa Newala walifanya maandamano wakiwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali kuhusu siku ya wanawake duniani ambayo yalianzia katika eneo la kituo cha mabasi Newala hadi viwanja vya mahakama ya mwanzo Newala mjini ambapo yalipokelewa na mgeni rasmi katika maadhimisho hayo Bi. Zuhura Farid akiwa na Mhe. Mkuu wa Wilaya ya Newala Bi. Aziza Mangosongo.
Akizungumza katika hotuba yake kwenye maadhimisho hayo, Bi. Zuhura Farid amewataka wanawake wazidi kushikamana, vikundi vya ujasiriamali wapewe elimu ya mapato na matumizi ili waweze kuendesha biashara zao vizuri pia wakipewa mikopo wafanye marejesho kama inavyotakiwa kwa kuwa Serikali ya awamu ya tano ikiongozwa na Rais John Magufuli inawasapoti wakina mama kwa kuwapa mikopo na wanarejesha bila riba.
Pia wanawake wa Newala walitakiwa kusheherekea siku hiyo kwa kuzingatia chanzo cha sherehe hizo ambacho ni kutetea haki za wanawake. Pia wanawake wametakiwa kuzingatia maadili kwao na katika malezi kwa kuzungumza na watoto mara kwa mara, kutumia lugha nzuri katika mawasiliano, kujenga urafiki na walimu ili kujua mienendo ya watoto wao shuleni.
"Nasisitiza jamii kubadili fikra hasi juu ya wanawake na kudumisha usawa wa kijinsia." Alisema Bi. Zuhura Farid.
Kauli mbiu ya maadhimisho ya siku ya wanawake duniani kwa mwaka huu 2020 ni "Kizazi cha usawa kwa maendeleo ya Tanzania ya sasa na ya baadaye".
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa