Mkuu wa Wilaya ya Newala Mhe. Mwangi Rajab Kundya leo tarehe 13/07/2021 amekutana na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa chuo ualimu Kitangari.
Mkuu wa Wilaya ya Newala Mhe. Mwangi Rajab Kundya akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Kundya amewataka watumishi hao kuwa wabunifu katika utendaji wao wa kazi kwa kuhakikisha kazi zao zinaleta matokeo bora kwa jamii katika kipindi chote wanachowatumikia wananchi.
"Utendaji wako wa kazi hautapimwa kwa kuwepo kwako kazini kwa muda mrefu au wingi wa vyeo ulivyowahi kushika, bali utapimwa kwa matunda bora yaliyopatikana katika kipindi chako ulichokuwa kazini." Alisema Mhe. Kundya.
Pia Mhe. Kundya ametumia nafasi hiyo kuwakumbusha watumishi kuwa ugonjwa korona upo hivyo wafanye kazi huku wakichukua tahadhari kwao na kwa watu wanaoshi nao kwa kuwa na utaratibu wa kuweka sehemu za kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni ili kujiepusha na virusi hivyo ya korona.
"Nawakumbusha ugonjwa wa korona upo, twendeni tukafanye kazi ya kuwazoesha watu tunaowaongoza kuishi kwa tahadhari kwa kujenga tabia ya kuosha mikono kwa maji tiririka na sabuni, kuepuka mikusanyiko mikubwa isiyo na lazima.........kuwawezesha watu wetu kuzifahamu dalili za korona ili akimuona mtu mwenye dalili hizo amshauri haraka kuwaona wataalam wa afya."
"Nawaomba na kuwasihi katika ofisi zetu, katika shule zetu tuanzishe utaratibu wa kuwa na sehemu za kuosha mikono kwa maji tiririka na sabuni, tukifanya hivyo tutaepuka na korona na magonjwa ya tumbo na kuharisha." Alisema Mhe. Kondya.
Wakati huo huo, Mhe. Kondya pia amewataka watumishi hao kushiriki katika kuhakikisha ulinzi na usalama wa jamii zetu kwa kuimarisha mfumo wa ulinzi kwa jamii ili pale watakapohisi kuna uvunjifu wa amani waweze kutoa taarifa mapema katika vyombo vya ulinzi na usalama.
Pia watendaji wa vijiji wametakiwa kuyatumia madaftari ya wakazi kwa kuwaandikisha kila mtu anayefika kuishi katika eneo lake la utawala na kujua shughuli wanazofanya wakazi wa maeneo yao.
Kikao hicho cha Mhe. Mkuu wa Wilaya ya Newala kimehudhuriwa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Newala Bw. Daniel Zenda, wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Newala, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Mhe. Tamimu Ladda, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Bw. Duncan Thebas, Wakuu wa Idara na Vitengo wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala, Watendaji Kata, Waratibu elimu kata, Wakuu wa Vituo vya afya na zahanati na watendaji wa vijiji.
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa