Afisa elimu taaluma kutoka sekretariet ya Mkoa wa Mtwara Bw. Mahamoud Kambona, amefanya ziara ya kikazi katika Wilaya ya Newala siku ya Alhamisi tarehe 11 Aprili 2019 na kufanya kikao na watumishi wa idara za elimu msingi na sekondari za Wilaya ya Newala katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala.
Akizungumza na watumishi wa idara za elimu kutoka Halmashauri ya Mji na Wilaya ya Newala Bw. Kambona amewataka walimu kuacha kufanya kazi kwa mazoea ila kujituma na kushirikiana pia kuwa wabunifu na wafuatiliaji katika utendaji wao wa kazi ili kutokomeza daraja la sifuri katika matokeo ya mitihani ya kuhitimu kidato cha nne na cha sita.
Akiendelea kuzungumza kwenye kikao hicho, Bw. Kambona amewahimiza walimu hao kuwa na uadilifu na usimamizi makini katika miradi yote inayopelekwa kwenye shule zao; kuhakikisha hakuna mwanafunzi asiyejua kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK) kwa shule za msingi; kusimamia upatikanaji wa chakula shuleni kwa ajili ya wanafunzi; vitabu vilivyopelekwa kwenye shule vitumike kama inavyotakiwa; na walimu wafanye kazi kwa upendo na mshikamano pasipo kuwa na fitina baina yao.
Hii ni sehemu ya mkakati wa Sekretariet ya Mkoa wa Mtwara upande wa elimu katika kuboresha utendaji kazi wa ofisi ya elimu Mkoa wa Mtwara ambapo maafisa waliopo kwenye ofisi hiyo wamegawana Halmashauri za kuzilea kwa lengo la kuimarisha usimamizi wa utekelezaji wa shughuli za elimu na kukuza ufanisi katika utendaji kazi.
Ziara ya Bw. Kambona katika Wilaya ya Newala ilikuwa na lengo la kujitambulisha kwa watumishi wa idara za elimu zilizopo wilaya ya Newala kuwa yeye ndiye mlezi wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala na Halmashauri ya mji wa Newala katika maswala yote yanayohusu elimu ya msingi na sekondari.
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa