Mapato ya ndani ni moja ya vyanzo vya mapato vinavyoisaidia Halmashauri ya Wilaya ya Newala kujiendesha yenyewe kwa kuwezesha shughuli mbalimbali za idara na vitengo vya Halmashauri na miradi mbalimbali ya maendeleo kwa wananchi wa Wilaya ya Newala.
Kwa Halmashauri ya Wilaya ya Newala, ushuru wa mazao mchanganyiko ni moja kati ya vyanzo vikuu vya mapato. Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2017/2018, hali ya ukusanyaji mapato ya ushuru wa mazao mchanganyiko hasa mbaazi imeathirika kutokana na kukosa soko la zao hilo. Hali hii imesababisha wakulima kushindwa kuuza mazao yao na hivyo kupelekea kushindwa kupata ushuru unaotokana na zao hilo.
Akizungumza na wananchi kupitia baraza la madiwani lililofanyika tarehe 02/11/2017, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Bw. Mussa Chimae alieleza kupungua kwa mapato hayo kwa robo hii ya kwanza ya mwaka 2017/2018 kwa kulinganisha na robo ya kwanza ya 2016/2017 ambapo kwa robo hiyo ya mwaka 2016/2017 Halmashauri ilikuwa imekusanya Tsh. 118,742,500.00 zilizotokana na zao hili na kwa robo hiyohiyo kwa mwaka huu jumla ya makusanyo ni Tsh. 12,305,310.00 yakiwa na tofauti kubwa ya Tsh. 106,437,190.00.
Aliendelea kusisitiza kuwa, kupungua kwa viwango vya utozaji wa ushuru wa mazao mchanganyiko kutoka asilimia tano (5%) hadi asilimia tatu (3%) kwa mazao ya biashara na asilimia mbili (2%) kwa mazao ya chakula pia kumeathiri kwa kiasi kikubwa bajeti ya Halmashauri kwa kuwa tayari ilikwisha andaliwa kwa kuzingatia ushuru wa asilimia tano (5%). Bw. Chimae alisema kuwa hali hii itaathili pia sehemu ya shughuli ambazo zilitakiwa zitekelezwe kwa kutumia mapato ya ndani.
Hata hivyo ili kuendana na hali halisi ya mapato, Halmashauri inatarajia kupitia upya makisio ya mapato ya ndani ili yaendane na ada mpya za ushuru ifikapo mwezi Disemba, 2017.
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa