Wakazi wa kata ya Mkoma II na Nambali leo tarehe 09/07/2020 wamekubaliana kujenga bweni kwa ajili ya watoto wa kike katika shule ya Sekondari Mkoma ili kukomesha utoro na kukuza ufaulu kwenye mitihani.
Baadhi ya wazazi na wakazi wa kata ya Mkoma II na Nambali wakiwa kwenye mkutano na uongozi wa shue kujadili ujenzi wa bweni la wasichana shuleni hapo leo.
Makubaliano hayo yamefanyika katika mkutano wa wazazi na uongozi wa shule uliofanyika shuleni hapo ambapo wazazi wa kata zote mbili za Mkoma II na Nambali ambazo zinahudumiwa na shule hiyo wamekubaliana kuchangia shilingi elfu tano kwa kila kaya ambapo wanatarajia kukusanya jumla ya shilingi milioni kumi kwa ajili ya kuanza ujenzi huo ifikapo tarehe 31/08/2020.
Mkuu wa shule ya sekondari Mkoma II Bw. Daniel Lukuwi akizungumza na waliohudhuria mkutano wa kujadili ujenzi wa bweni la wasichana kwa lengo la watoto hao kukaa shuleni.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkuu wa Shule ya Sekondari Mkoma Bw. Daniel Lukuwi amesema kuwa, wazo la shule hiyo kujenga bweni kwa ajili ya wasichana limekuja baada ya wanafunzi wengi hasa wa kike kuwa watoro, kuacha shule na wengine kuahirisha masomo.
"Ufaulu wa wanafunzi unashuka sana kwa kuwa jamii hii ni ya kilimo cha kuhama, hivyo msimu wa kilimo cha ufuta wazazi huama makazi yao na kwenda Liwale Lindi, watoto wanaachwa bila usimamizi hivyo kupelekea baadhi kuwa watoro na watoto wengine husafiri na wazazi kwenda shambani hivyo kusimama masomo." Alisema Mwalimu Lukuwi.
Wakizungumza katika mkutano huo, wazazi waliupongeza uongozi wa shule kwa kuja na wazo la kujenga hosteli kwa kuwa itawasaidia watoto kubaki shuleni kipindi ambacho wazazi wanasafiri kwenda kulima ufuta mkoa wa Lindi.
Mkutano huo uliwahusisha wazazi na walezi wa wanafunzi, uongozi wa shule na, uongozi wa kata na vijiji pamoja na uongozi wa Halmashauri ambao uliwakilishwa na Afisa Elimu Sekondari Bw. Friday Sondasy na Afisa Ardhi na Maliasili Bi. Magreth Likonda ambapo jamii ya kata ya Mkoma II na Nambali iliahidi kuchangia kwa kila kaya na jumla ya shilingi laki tano na sitini na tano na ahadi ya mifuko kumi ya saruji zilitolewa.
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa