Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula leo Jumatano tarehe 28/07/2021 amewataka wakazi wa Newala na Masasi kuheshimu mipaka ya ardhi iliyowekwa ili kuepuka migogoro ya ardhi.
Mhe. Mabula ameyasema hayo katika kijiji cha Miyuyu, kata ya Chilangala, Wilaya ya Newala alipofika kusikiliza na kutatua mgogoro wa uhalisia wa mpaka wa ardhi kati ya Newala na Masasi unaotenganisha kijiji cha Miyuyu kilichopo Newala na kijiji cha Ndanda kilichopo Masasi.
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya makazi, Mhe. Angeline Mabula (wa kwanza kushoto) akipitia tangazo la Serikali kuhusu mpaka wa Newala na Masasi
Akizungumza katika ziara hiyo, diwani wa kata ya Chilangala Mhe. Nandonde Jamali Jaffu ameeleza kuwa malalamiko ya wananchi ni kuwa mipaka ya asili (ya kichifu) haikuzingatiwa wakati wa kuandaa ramani za vijiji na kuweka mipaka ya Wilaya hivyo wananchi hawakubaliani na mipaka iliyopo kwenye ramani.
Aidha, Mhe. Mabula ameelekeza Wakurugenzi kwenda kwenye maeneo yote yenye migogoro na kuwasilikiliza wananchi kujua changamoto yao ni nini, na wakishakubaliana, ofisi ya ardhi itatekeleza kwa kuweka mawe ya mipaka kwa mujibu ya makubaliano yao.
"Naagiza Wakurugenzi wote wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala na Halmashauri ya Mji Masasi kwenda kwenye vijiji vyenye migogoro kuwakutanisha wananchi wa vijiji husika vilivyopo mpakani, chukueni ramani na tangazo la Serikali (GN) lililotolewa la vijiji husika na muwasomee ili waelewe vizuri". Alisema Mhe. Mabula.
Mhe. Mabula amewaeleza wananchi kuwa mipaka haiwazuii wananchi kufanya shughuli zao za kiuchumi ilimradi watafuata taratibu zote za matumizi bora ya ardhi yaliyowekwa katika eneo husika.
Mhe. Mabula ameeleza kuwa, mipaka inayotambulika kwa sasa ni ile iliyopo kwenye ramani na iliyotolewa kwenye tangazo la Serikali na iwapo wananchi watataka marekebisho wanatakiwa kufuata taratibu za awali zilizotumika kuandaa mipaka hiyo.
Ziara hiyo ya Mhe. Mabula ni utekelezaji la agizo lililotolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Philip Mpango alilolitoa akiwa kwenye ziara Wilayani Newala siku ya Jumapili tarehe 25/07/2021 akimuagiza Mhe. Mabula kubaki Newala ili kushughulikia mgogoro wa ardhi uliowasilishwa na Mbunge wa jimbo la Newala Vijijini Mhe. Maimuna Mtanda.
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa