Mkuu wa mkoa wa Mtwara Gelasius Byakanwa amefanya ziara ya kusikiliza kero, changamoto na maoni kutoka kwa wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala siku ya Ijumaa tarehe 10/05/2019 kupitia mkutano wa hadhara uliofanyika katika ofisi ya kata ya Kitangari, Wilaya ya Newala.
Kupitia mkutano huo, mkuu wa mkoa ameweza kupokea kero na changamoto mbalimbali za wananchi zikiwemo ucheleweshwaji wa utoaji wa hukumu za kesi katika mahakama ya mwanzo, tabia za wafanyabiashara kuuza dawa za kupulizia mikorosho kiholela, madai ya fedha za uzalishaji wa miche ya mikorosho kwa msimu wa mwaka 2017/2018, madai ya baadhi ya wakulima wa chama cha msingi Chemana kuhusu malipo ya korosho za msimu wa 2017/2018, upimaji wa ardhi, ukosefu wa maji, ukosefu wa umeme na ubovu wa miundombinu ya barabara huku wakuu wa idara husika wakitakiwa kutoa majibu na ufafanuzi juu ya kero na changamoto hizo.
Akiendelea kuzungumza na wananchi wa Newala, Byakanwa amewataka wajasiriamali kuwa na vitambulisho vya ujasiriamali vilivyotolewa na Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Joseph Magufuli. "Mhe Rais amekusudia kuwasaidia wajasiriamali wenye kipato cha chini ambao faida inayotokana na biashara zao haifikii shilingi milioni nne kwa mwaka kwa kuwapatia vitambulisho vya ujasiriamali ili kuwaondolea hali ya ulipaji wa kodi za mara kwa mara na badala yake walipie shilingi elfu ishirini tu kwa mwaka" alisema Byakanwa.
Mikutano hiyo ya kusikiliza kero ni moja ya njia anayoitumia Byakanwa kukutana na wananchi wa mkoa wake na kushughulikia matatizo waliyonayo ikiwa pia ni utekelezaji wa agizo la Mhe Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania kwa viongozi wa mikoa yote kuzifahamu na kusaidia kutatua kero za wananchi.
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa