Mafunzo yanayohusu DHFF, CHF iliyoboreshwa pamoja na mfumo wa JAZIA (PVS) kwa ngazi ya Halmashauri, yanayolenga kuwajengea uwezo watendaji wa kamati za afya, ili kuimarisha uelewa wa pamoja unaolenga kupeleka maelekezo sahihi katika vituo vya kutolea huduma za afya na jamii kwa ujumla, yamefunguliwa rasmi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo ya siku tatu yaliyoanza tarehe 7/5/2018 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Bw. Mussa Chimae, amesema lengo mahususi la mafunzo hayo ni kuelewa kwa upana maana ya ugatuaji wa mipango ya afya na bajeti kwa utaratibu wa kupeleka fedha moja kwa moja kwenye vituo vya kutolea huduma (DHFF), yenye matarajio ya kupunguza urasimu na kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa kuimarisha uwajibikaji na uboreshaji wa uandaaji wa mipango, bajeti na matumizi yanayolenga kuboresha huduma za afya.
Bw. Chimae ameongeza kuwa, dhana kubwa ya serikali ni kuwashirikisha wananchi ili kujua changamoto zinazowakabili, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha huduma za afya hususani upatikanaji wa dawa, ziwe zinapatikana kwa wakati, na sio kuzorotesha huduma, kwani lengo ni upatikanaji wa dawa na huduma nyingine za afya uwe wa asilimia 100% na sio asilimia 96% tena.
Serikali ya awamu ya Tano, imedhamiria kuboresha huduma za afya kwa wananchi wake kwa kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa watu wote na kwa gharama nafuu, ikiwa ni pamoja na kubuni na kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuboresha huduma za afya kwa kukarabati vituo vya afya, kuboresha takwimu za afya na kuongeza ufanisi wa uandaaji wa mipango, bajeti na kuongeza mapato hususani katika ngazi ya mamlaka za Serikali za mitaa, ikiwemo halmashauri ya Wilaya ya Newala.
Washiriki wa mafunzo yahusuyo DHFF na CHF iliyoboreshwa wakiwa katika siku ya kwanza ya mafunzo kwa ngazi ya Halmashauri yaliyofanyika jumatatu ya tarehe7/5/2018 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala.
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa