Halmashauri ya Wilaya ya Newala siku ya jana Ijumaa, tarehe 04/12/2020 imefanya mkutano wake wa kwanza wa baraza la madiwani tangu ufanyike Uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani mwezi Oktoba mwaka huu 2020.
Akizungumza katika mkutano huo wa baraza la madiwani, mgeni rasmi katika mkutano huo ambaye ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara Bw. Alphayo Kidata alianza kwa kuwaeleza madiwani juu ya uhusiano wa kimadaraka na kimajukumu kati ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa kwa lengo la kumuhudumia mwananchi wa kawaida.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara Bw. Alphayo Kidata (aliyesimama) akizungumza katika mkutano wa baraza la madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Kutoka upande wa kushoto ni Mbunge wa jimbo la Newala Mhe. Maimuna Mtanda, na kulia ni mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Mhe. Ladda Mfaume Tamimu.
Pia Bw. Kidata aliwakumbusha madiwani majukumu yao ya msingi wanayotakiwa kuyafanya kama wawakilishi wa wananchi.
"nyinyi mmetumwa na wananchi, wamewachagua, kwa hiyo nyinyi ni wawakilishi wa wananchi wote wa kata zenu katika Halmashauri hii. Kwa njia hiyo na msingi huo, hoja zozote utakazokuwa unazileta Mheshimiwa diwani kwenye baraza la Halmashauri ni hoja ambazo umeshirikishana na wananchi wako wakakutuma uzilete na siyo ulete hoja zako binafsi." Alisema Bw. Kidata.
Bw. Kidata pia amewataka madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala kuwa waaminifu katika kipindi chote cha utawala wao kwa kuwa wananchi wa jimbo la Newala vijijini wana imani sana nao na wamewakabidhi ndoto zao, na hilo ni deni kubwa sana kwao.
Aidha, Mhe. Mbunge wa jimbo la Newala vijijini Bi. Maimuna Mtanda pia alitumia mkutano huo wa baraza la madiwani kuwashukuru wananchi wa jimbo la Newala vijijini wote kwa kukiamini Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kumchagua kwa kishindo Mhe. Rais, yeye Mbunge pamoja na waheshimiwa madiwani.
"Tunawashukuru wana Newala wote kwa kazi nzuri, kwanza wamempa kura nyingi Mhe. Rais, lakini pia kwa kukiamini Chama Cha Mapinduzi na kukipa ushindi uliotukuka." Alisema Mhe. Mtanda.
Mhe. Mtanda ameahidi kuwa yeye na waheshimiwa madiwani watatoa ushirikiano wa kutosha katika maeneo yote kwa viongozi wa dini, watumishi wa umma na wananchi wote ambao wanatakiwa kuwahudumia.
Wakati huohuo, Mkuu wa Wilaya ya Newala, Mhe. Aziza Mangosongo amewataka waheshimiwa madiwani wote kusoma vizuri kanuni, sheria na taratibu za Halmashauri na kutekeleza majukumu yao kwa kutekeleza vyema ilani ya Chama Cha Mapinduzi.
"Haijalishi wewe ni mwanachama wa chama gani, hapa tunataka wewe utekeleze ilani ya chama kinachotawala, Chama Cha Mapinduzi." Alisema Mhe. Mangosongo.
Mhe. Mangosongo pia amewataka madiwani wote kwenda kuanzisha miradi mipya ya maendeleo na kuiendeleza miradi ya zamani katika kata zao.
"Tusibuni wenyewe miradi kichwani, tuwashirikishe wananchi na watendaji katika kata zetu." Alisisitiza Mhe. Mangosongo.
Mkutano huo wa baraza la madiwani umefanyika kwa siku moja katika ukumbi wa mikutano wa chuo cha walimu Kitangari na ulihudhuriwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Bw. Duncan Thebas, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara Bw. Alphayo Kidata, Mkuu wa Wilaya ya Newala Mhe. Aziza Mangosongo, wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Newala, Mhe. Mbunge wa jimbo la Newala vijijini Bi. Maimuna Mtanda, viongozi wa vyama vya siasa vya CCM na ACT wazalendo wilaya ya Newala, viongozi wa dini,maafisa wa Maadili Sekretariet ya Maadili ya viongozi wa umma kanda ya Kusini, Hakimu Mkazi wa wa Wilaya ya Tandahimba Mhe. Nasra Mkadam Mwinshehe, waheshimiwa madiwani, wakuu wa idara na vitengo, wageni waalikwa na waandishi wa habari.
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa