Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe.Gelasius Byakanwa ametambulisha rasmi kampeni ya "Shule ni Choo" kwa Wilaya ya Newala siku ya Ijumaa tarehe 20/09/2019.
Kampeni hiyo ya "Shule ni Choo" ni njia anayoitumia Mhe. Byakanwa kuhakikisha vinajengwa vyoo vya wanafunzi na walimu kwenye shule zenye uhaba wa vyoo kwa kutumia michango inayotolewa na wadau mbalimbali wakiwemo watumishi wa umma waliopo kwenye maeneo husika, viongozi, wakuu wa taasisi mbalimbali na wananchi wote.
Akitambulisha kampeni hiyo, kwenye kikao na watumishi, madiwani wa Halmashauri wa Wilaya na Mji wa Newala, wakuu wa taasisi mbalimbali na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya, Mhe. Byakanwa ameeleza kuwa katika baadhi ya maeneo ambapo zimejengwa shule, vimejengwa vyumba vya madarasa tu badala ya majengo yote yanayohitajika ili kukidhi uwepo wa shule. Hivyo ameamua kuja na kampeni hiyo baada ya kuona uhaba mkubwa wa matundu 6547 ya vyoo vya wanafunzi na 1830 ya vyoo vya walimu kwenye shule za msingi zilizopo kwenye mkoa wote wa Mtwara.
Katika kuunga mkono kampeni ya "Shule ni Choo" jumla ya ahadi za shilingi milioni kumi na laki tatu pamoja na mifuko mia sita na sabini na tisa ya saruji zilitolewa katika harambee iliyoitishwa na Mhe. Byakanwa kwenye kikao hicho.
Mbali na kampeni hiyo, Mhe. Byakanwa pia alisisitiza juu ya utekelezaji bora wa sheria ya mipango miji, kuujenga mji wa Newala na kuwekeza katika sekta mbalimbali, na kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika tarehe 24/11/2019.
Kampeni ya "Shule ni Choo" inatarajiwa kuzinduliwa rasmi tarehe 12/10/2019 Mkoani Mtwara na mgeni rasmi katika uzinduzi huo anatarajiwa kuwa Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Mhe. Benjamin William Mkapa.
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa