Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi Wilayani Newala imeridhishwa na hali utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambayo inatekelezwa katika halmashauri ya Wilaya ya Newala.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa CCM Wilayani Newala Mzee Jabiri Mohamedi Mtanda alipokuwa katika ziara ya siku moja ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo iliyofanyika tarehe 15/05/2018 katika maeneo ya Makukwe, Lengo, Mnyambe, Kata mpya ya Muungano na Kitangari.
Mzee Mtanda ambae pia ndiyo mwenyekiti wa kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi Wilayani Newala, amesema wamefanya ziara hiyo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Irani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi na kwamba miradi yote waliyoitembelea ipo katika hatua nzuri ya utekelezaji, jambo linaloleta matumaini makubwa katika matumizi sahihi ya fedha za miradi hiyo ambayo kimsingi inatekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Newala.
Ziara hiyo ilihusha miradi mbalimbali ya maendeleo, ukiwemo Mradi wa ujenzi wa vyumba vitano vya madarasa katika Shule ya Sekondari Makukwe, ambapo tayari Halmashauri ya Wilaya ya Newala kupitia mfuko wa Elimu imeshatoa shilingi 75,000,000/= (Millioni 75) na hadi kukamilika kwa ujenzi huo wa vyumba vitano vya madarasa, mradi utagharimu kiasi cha shilingi 85,600,000/= (Milioni 85 na laki sita) zikiwemo shilingi 83,000,000/= (milioni 83) kutoka mfuko wa elimu, na shilingi 2,100,000/= (milioni 2 na laki 1) ni kutokana na nguvu za wananchi.
Pichani ni vyumba vitatu kati ya vyumba vitano vya madaarasa ya shule ya sekondari Makukwe, Mradi ambao mpaka sasa upo katika hatua ya umaliziaji, ulianza mwezi Februari, 2018 na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Mei mwaka huu wa 2018.
Mradi mwingine ni wa ujenzi wa nyumba 6 kwa 1 (six in one) za walimu katika shule ya sekondari Lengo, na hadi kukamilika utagharimu kiasi cha shilingi 143,500,000/= (milioni 143 na laki 5) zikiwemo shilingi 141,000,000/= (milioni 141) kutoka mamlaka ya elimu Tanzania (TEA), na nguvu za wananchi kiasi cha shilingi 2,500,000/= (milioni 2 na laki 5) ambao pia wameshiriki kazi za kusafisha eneo la mradi, kujaza msingi vifusi na kukusanya mchanga.
Kamati ya Siasa ya CCM - Newala wakikagua mradi wa ujenzi wa nyumba 6 za walimu (Six in One) katika shule ya Sekondari Lengo ambao pia ulianza mwezi Februari, 2018, na unatarajiwa pia kukamilika ifikapo mwezi Mei mwaka huu wa 2018.
Mradi mwingine ni mradi wa ujenzi wa Bwalo la chakula na jiko katika shule ya sekondari Mnyambe, ambapo fedha za mradi huu zilizoletwa na Serikali kupitia Wizara ya Elimu ni shilingi 100,000,000/= (mradi wa EP4R). Bwalo hili litakuwa ni la kisasa ambalo si kwaajili ya chakula tu, bali litatumika pia kama ukumbi wa kufanyia mitihani, mikutano, mdahalo na burudani kwa wanafunzi, hivyo kwa ujumla bwalo hilo likikamilika litaongeza hadhi ya shule hiyo ya Sekondari ya Mnyambe.
Hata hivyo fedha zilizoletwa shilingi milioni 100, kulingana na mwenendo wa matumizi ya fedha za mradi huu, kiasi hiki hakitatosha kuukamilisha maana mpaka sasa tayari zimetumika shilingi 72,000,000/= hivyo mawasiliano na mhandisi wa ujenzi yameshafanyika ili kuona utafikia wapi na upungufu utakuwa kiasi gani.
Mradi wa Ujenzi wa Bwalo la chakula na jiko katika shule ya sekondari Mnyambe ambao usimamizi wake unafanywa na Bodi ya shule pamoja na uongozi wa Serikali ya Kata kwa kuzingatia maelekezo ya wataalamu ulianza mwezi Februari, 2018 na unatarajiwa kukamilika mwezi juni, 2018.
Aidha katika shule hiyo ya Sekondari Mnyambe, kuna changamoto ya nyumba 16 za walimu, ambapo kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018 Serikali ilitenga bajeti ya shilingi 70, 000,000/= (milioni 70) ambazo serikali imeahidi kuwa zitaingia mwishoni mwa mwezi Mei mwaka huu, ili kujenga nyumba 2 za walimu yaani (2 in 1).
Mradi mwingine ni mradi wa ujenzi wa chumba kimoja cha darasa katika shule ya Msingi Muungano ambao ulianzishwa na jamii mwezi Juni, 2016 kupitia mkutano maalum. Mwaka 2017 shule ilipokea vifaa vya ujenzi na fedha taslimu shilingi 1,350,000/= kutoka mfuko wa Jimbo Newala kwa lengo la kumalizia ujenzi huo ambao kwa sehemu kubwa ya awali ulitekelezwa kwa nguvu za wananchi wa Kata mpya ya Muungano.
Pichani ni mradi wa chumba kimoja cha darasa katika shule ya msingi Muungano ambao kwasasa umeshakamilika.
Mradi mwingine ni wa uboreshaji wa huduma za maji Tarafa ya Kitangari na vijiji jirani ambapo kwasasa Serikali inajenga Tanki la Maji la lita 250,000/= katika kijiji cha Nanda kilichopo Kata ya Kitangari, ambao unatekelezwa kwa awamu ya tatu, awamu ya kwanza inahusisha ujenzi wa Tanki la Lita 250,000, na ulazaji wa Bomba la kipenyo cha inchi 8 yenye urefu wa 400m, Awamu ya pili inahusisha ujenzi wa bomba lenye kipenyo cha inchi 3 yenye urefu wa 3km, ujenzi wa vilula kwenye mitaa na awamu ya tatu inahusisha kuwaunganisha wateja wa majumbani.
Mradi huu umeweza kufanyika kutokana na bakaa iliyobaki kwenye mradi wa maji wa Mapili ambao ulizinduliwa na Mhe.Waziri wa Maji na Umwagiliaji tarehe 17/01/2018, na unajengwa na mkandarasi JECE & NAMIS CORPORATE LTD.
Pichani ni Mhandisi Nsajigwa Sadick akitoa taarifa ya mradi wa ujenzi wa Tanki la maji la lita 250,000 kwa kamati ya Siasa ya CCM- Newala wakati wa ukaguzi wa mradi huo.
Mabomba ya kipenyo cha inchi 8 yenye urefu wa 400m, ambayo yanatarajiwa kulazwa kwa awamu ya kwanza ili kuboresha upatikanaji wa maji katika Kata ya Kitangari na vijiji jirani.
Kukamilika kwa mradi huu kunatarajia kugharimu kiasi cha shilingi 100,263,400/= kwa mujibu wa mkataba, na hadi sasa mkandarasi tayari amelipwa kiasi cha shilingi 80,263,400/= na unatarajiwa kukabidhiwa tarehe 30/09/2018.
Mradi mwingine ni mradi wa upanuzi wa miundombinu majengo ya kituo cha Afya Kitangali unaogharimu jumla ya shilingi milioni 400, unahusisha ujenzi wa nyumba moja ya mtumishi wa kituo hicho na kuboresha huduma za upasuaji, maabara na huduma ya damu salama, chumba cha kuhifadhia maiti, wodi ya wazazi na watoto, kichomea taka, ikiwa ni pamoja na kupunguza vifo na rufaa za kina mama wajawazito ambao walikuwa wanalazimika kukimbizwa hospitali ya Mji Newala.
Moja kati ya sehemu ya mradi wa upanuzi wa miundombinu majengo katika kituo cha Afya Kitangari ambao upo katika hatua ya umaliziaji.
Aidha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo unakabiriwa na changamoto kuu mbili ambazo ni pamoja na ushiriki mdogo wa wananchi katika kujitolea kusaidia shughuli za ujenzi wa miradi, na ucheleweshwaji wa fedha za utekelezaji wa miradi hiyo, hivyo kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi Wilayani Newala inaiomba serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Newala kuharakisha mchakato wa fedha za miradi ya maendeleo ili utekelezaji wake uweze kufanywa kwa wakati uliokusudiwa, na uondoe adha iliyokuwepo kutokana na kukosekana kwa mradi huo katika sehemu husika.
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa