Halmashauri ya Wilaya ya Newala imefanikisha uendeshaji wa zoezi la ugawaji wa dawa za tiba na kinga dhidi ya magonjwa yasiyopewa kipaumbele siku ya Ijumaa tarehe 03/05/2017.
Zoezi hilo lilihusisha watoto wenye umri wa kuanzia miaka mitano hadi kumi na nne wanaosoma na wasiosoma shule na liliendeshwa katika shule zote za msingi zilizopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Newala.
Mwalimu wa afya akimpatia dawa mwanafunzi wakati wa zoezi la ugawaji wa dawa za magonjwa yasiyopewa kipaumbele
Dawa zilizotolewa ni Albendazole kwa ajili ya kutibu na kukinga minyoo ya tumbo na Praziquantel kwa ajili ya kutibu na kukinga kichocho.
Aidha walimu pamoja na watoto waliopewa dawa hizo wamepongeza Serikali kwa kuwawezesha kupata kingatiba hiyo kwa kuwa itawawezesha watoto kuwa na afya bora na hivyo kuhudhuria vyema masomo na kupata elimu.
Magonjwa yasiyopewa kipaumbele ni magonjwa ambayo yamo ndani ya jamii yenyewe na hata wataalamu husika ama viongozi hawayapi umuhimu kulingana na madhara yake katika jamii. Magonjwa hayo ni pamoja na matende na mabusha, kichocho, minyoo ya tumbo, usubi na tarakoma.
Kwa Halmashauri ya Wilaya ya Newala jumla ya watoto 26,715 walitarajiwa kupatiwa dawa hizo ambazo ni kingatiba kwa ajili ya magonjwa hayo.
Zoezi la ugawaji wa dawa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Newala lilifanyika kwa ufadhili wa Wizara ya Afya ikishirikiana na shirika la IMMA World Health.
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa