Afisa kilimo, Umwagiliaji na Ushirika wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Bw. Alfod Mpanda, amewataka wakulima wote Wilayani Newala kujihusisha na kilimo cha Alizeti kwa wingi, na kwamba walitambue zao hilo kuwa ni muhimu kama wanavyolitambua zao la korosho.
Bwana Mpanda ameyasema hayo alipokuwa anaongea na wakulima wa kijiji cha Mtopwa, katika hafla fupi ya tathmini ya shamba darasa la Alizeti, iliyofanyika tarehe 24/05/2018 katika shamba la wanakikundi cha VICOBA, lililopo kijiji cha Mtopwa Kata ya Mtopwa.
Katika hafla hiyo, Bwana Alfodi Mpanda ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi, amesema zao la Alizeti ni moja kati ya mazao muhimu sana hapa nchini, ambayo yanatambulika katika Nyanja tofauti tofauti, ikiwemo ya chakula na biashara, ambayo kwa hakika limeleta mafanikio makubwa kwa wakulima wa zao hilo, hasa katika maeneo ambayo wameanza siku nyingi kujihusisha na kilimo cha zao la Alizeti, na kwamba upo uwezekano mkubwa kwa wakulima wa Wilaya ya Newala, kubadilika na kujihusisha pia na kilimo cha Alizeti, ili iwe chachu ya maendeleo yao na Wilaya kwa ujumla.
Nae Mkurugenzi wa Aga Khan Foundation Bw. Biko Evarist, amesema shirika la Aga Khan, lina nia nzuri ya kushirikiana kwa karibu na wakulima pamoja na wadau wa kilimo hususani wa kilimo cha Alizeti, ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowakabili, na kwamba wapo tayari kuhakikisha wakulima wengi wanakuwa na mashamba yao binafsi, na sio ya vikundi tu.
Wakati huo huo Diwani wa Kata ya Mtopwa Mhe. Anafi Nahonyo, amelishukuru shirika la Aga Khan Foundation kwa ushirikiano wao mkubwa na wakulima kupitia Idara ya Kilimo, na amewaomba wazidi kutoa elimu zaidi juu ya zao la Alizeti kwa maafisa ugani wengi, ili waweze kuwasaidia wakulima wengine wenye nia na zao hilo, huku pia akiziomba Taasisi zinazohusika na uuzaji wa mbegu ya Alizeti, kupunguza bei ya zao hilo, ili wakulimawengi zaidi wapate unafuu wa kununua mbegu hizo za Alizeti
Mafanikio ya wakulima wa zao la Alizeti Wilayani Newala yameanza kujionyesha kwa wanakikundi cha VICOBA cha AMKENI “A” kilichopo kijiji cha Mtopwa Kata ya Mtopwa, ambapo katibu wa kikundi hicho chenye jumla ya hekari 3 za za shamba la Alizeti Bi Salama Mohamedi Mnihauke, amesema kwa mwaka uliopita kikundi hicho kiliweza kupata jumla ya Tsh 400,000/= (laki nne) kutokana na zao la Alizeti, ambapo 320,000/= zilipatikana baada ya kukamua viroba 8 vya Alizeti na kuuza lita 80 za mafuta ya Alizeti, na shilingi 80,000/= zilipatikana baada ya kuuza mashudu ya Alizeti kwa msimu uliopita, na hivyo kupata jumla ya shilingi laki nne tu, na kwamba kutokana na matarajio mazuri waliyonayo kwa shamba hilo, upo uwezekano mkubwa wa kufanikiwa zaidi katika mavuno ya msimu huu.
Katika hatua nyingine Afisa maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Bi Christina Kambuga, amesema Halmashauri kwa kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii, ipo tayari kuhamasisha zaidi wananchi katika kulima zao la Alizeti, ili waweze kupata masoko zaidi, ikiwa ni pamoja na kusaidia kuibadilisha jamii, ianze sasa kutumia mafuta ya Alizeti, ambayo ni salama zaidi kwa Afya zao.
Pichani ni Afisa Kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Bw. Alfodi Mpanda (wa katikati kulia) akitoa ufafanuzi kwa wananchi juu ya kilimo cha zao la Alizeti wakati wa tathmini ya shamba darasa iliyofanyika tarehe 24/05/2018 katika kijiji cha Mtopwa kilichopo Kata ya Mtopwa Wilayani Newala.
Ziara ya Tathmini ya shamba darasa la zao la Alizeti iliyoandaliwa na shirika la Aga Khan Foundation kwa kushirikiana na Idara ya Kilimo ya Halmashauri ya Wilaya ya Newala, iliyohusisha wakulima wa Tandahimba, Nanyamba na Newala, imekamilika jana tarehe 24/05/2018 katika kijiji cha Mtopwa Wilayani Newala, baada ya kutokea Wilaya za Ruangwa, Nachingwea na Masasi Mkoani Mtwara.
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa