Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Mhe. Mfaume Ladda jana tarehe 16/03/2021 amezindua maadhimisho ya wiki ya maji Wilaya ya Newala kwa kushirikiana na wananchi wa Newala kufanya usafi wa mazingira na kupanda miti katika chanzo cha maji Mitema kilichopo katika kijiji cha Mitema, Halmashauri ya Wilaya ya Newala.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Mhe. Mfaume Tamimu Ladda akizungumza siku ya uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya maji Wilaya ya Newala katika kijiji cha Mitema.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mhe. Ladda ameeleza kuwa wiki hii ya maji ina lengo la kujenga uelewa na kuhamasisha umma juu ya mipango na mageuzi yanayoendelea ya sekta ya maji na umuhimu wa ushiriki wa kila mdau katika mipango ya usafi wa mazingira na usambazaji wa maji. Hivyo kuwataka wana jamii kutunza mazingira katika vyanzo vya maji ili kuwa na huduma za maji endelevu.
"Katika kutekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi, Serikali ya awamu ya tano imefanya maboresho ya kuunda wakala wa maji na usafi wa mazingira Vijijini (RUWASA) ambao kwa wiki hii ya maji wamejipanga kupanda miti katika maeneo jirani na vyanzo vya maji; kufanya usafi katika maeneo ya matenki na vyumba vya pampu; na kufanya mafunzo kwa jumuiya za watumia maji na kuweka mawe ya msingi katika miradi ya Chitandi na Chiule." Alisema Mhe. Ladda
Wananchi wa Mitema wakishiriki kupanda miti katika maeneo ya chanzo cha maji Mitema siku ya uzinduzi ya maadhimisho ya wiki ya maji Wilaya ya Newala.
Kwa wakati mwingine akizungumza katika uzinduzi huo, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Newala, Mhandisi Nsajigwa Sadiki, amesema kuwa maadhimisho ya wiki ya maji Wilaya ya Newala kwa mwaka huu 2021 yatajikita katika kuonyesha thamani ya maji katika nyanja za kijamii na kiuchumi yakienda sambamba na uzinduzi wa miradi ya maji iliyokamilika na uwekaji wa mawe ya msingi.
Meneja wa RUWASA Wilaya yaNewala, Mhandisi Nsajigwa Sadiki akizungumza na wananchi siku ya uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya maji Wilaya ya Newala
"Lengo kuu la kuweka mawe ya msingi katika maadhimisho ya wiki hii ya maji ni kutumia fursa hii kuonesha mafanikio ya Wizara ya Maji kwa vitendo na namna ambavyo huduma ya majisafi na usafi wa mazingira imeweza kuboreshwa nchini kwa kipindi kifupi." Alisema Mhandisi Nsajigwa.
Kila mwaka nchini Tanzania wiki ya maji huadhimishwa kuanzia tarehe 16 mpaka 22 mwezi Machi, kwa lengo la kuungana na mataifa mengine duniani katika kutathmini utekelezaji, mafanikio, changamoto na kuainisha mikakati ya kuboresha na kuimarisha utoaji wa huduma ya maji safi na usafi wa mazingira na kutunza usimamizi wa rasilimali za maji nchini.
Kauli mbiu ya maadhimisho ya wiki ya maji kwa mwaka huu 2021 ni "Thamani ya maji kwa uhai na maendeleo."
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa