Benki ya CRDB kupitia Tawi la Newala imekabidhi madawati 40 yenye thamani ya shilingi milioni 4 kwa Shule ya Sekondari Chitekete, iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Newala mkoani Mtwara, kupitia mpango wake wa kijamii wa “Keti Jifunze”. Msaada huo umetolewa kwa lengo la kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi, huku ukilenga kupunguza changamoto ya uhaba wa madawati mashuleni.
Mpango wa Keti Jifunze ni moja ya mikakati ya Benki ya CRDB ya kusaidia maboresho ya elimu kwa shule za serikali kwa kutoa viti, meza na vifaa vingine muhimu vya kujifunzia. Mpango huu ni sehemu ya mchango wa benki hiyo katika kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita ambayo imeendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya elimu, hususan miundombinu na vifaa vya kufundishia.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo katika Hafla iliyofanyika tarehe 1 Agosti 2025 Shuleni hapo, Meneja Biashara wa CRDB Kanda ya Kusini, Bw. Emmanuel Biganio alisema mpango wa Keti Jifunze umefikia awamu ya tatu na unalenga kutoa madawati katika halmashauri 185 nchini kote. Kwa Kanda ya Kusini pekee, zaidi ya madawati 450 yanatarajiwa kusambazwa kwa shule zilizochaguliwa, ambapo Sekondari ya Chitekete ni miongoni mwa walionufaika.
“Sisi kama wadau, kama wananchi wa Tanzania na taasisi inayofaidika na utulivu wa nchi hii, hatuwezi kukaa kimya. Kupitia taasisi yetu, tumeamua kuchangia maendeleo haya kwa kutoa madawati kwenye shule za serikali, tukianza na halmashauri 185 nchini kote,” alisema Bw. Biganio.
Msaada huo ulipokelewa rasmi na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala, Bi. Magreth Likonda, ambaye aliishukuru benki ya CRDB kwa kuonesha mshikamano na ushirikiano wa dhati na serikali katika kuleta maendeleo ya elimu kwa vitendo. Alieleza kuwa msaada huo utachangia kuongeza ari ya walimu kufundisha na wanafunzi kujifunza katika mazingira bora zaidi.
Hafla ya kukabidhi msaada huo ilihudhuliwa na Viongozi Serikali ya Kijiji cha Chitekete , Wananchi,Walimu na Maafisa Elimu ngazi ya kata na Halmashauri.
@mtwarars_habari
@ortamisemi
@msemajimkuuwaserikali
@gersonmsigwa
@samia_suluhu_hassan
Kitangari,Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa