Kila tarehe 26 ya mwezi wa nne, Tanzania huazimisha siku ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa namna tofauti tofauti kwa kila eneo.
Kwa mwaka huu wa 2018, maadhimisho haya yamefanyika kitaifa Mkoani Dodoma, huku kila mkoa na Wilaya nazo zikiazimisha siku hiyo kwa namna tofauti tofauti kama ilivyo ada.
Kwa upande wa Wilaya ya Newala, Wananchi wamesherehekea maadhimisho ya siku ya Muungano kwa kufanya usafi katika maeneo mbalimbali ya mjini na vijijini.
Halmashauri ya Wilaya ya Newala inayoongozwa na Mkurugenzi wake Bw. Mussa Chimae,wameshirikiana na wananchi wa tarafa ya Kitangari kufanya usafi katika eneo la upanuzi wa miundombinu ya kituo cha afya Kitangari siku ya alhamisi tarehe 26/04/2018, zoezi hilo lilianza mnamo saa 12 likiongozwa na Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Newala hadi majira ya saa nne za asubuhi ambapo maeneo yote katika kituo hicho cha afya yaliweza kufanyiwa usafi ikiwa ni pamoja na kushirikiana kusaidi kupanga vizuri matofari ili ujenzi uendelee katika eneo hilo.
Zoezi hilo la kufanya usafi kituo cha afya Kitangari limefanyika ipasavyo siku ya maadhimisho ya Muungano ikiwa ni moja kati ya njia za ushirikishaji wananchi kujitolea kushiriki katika shughuli za maendeleo ya kata, kijiji na Wilaya kwa ujumla.
Tanganyika na Zanzibar ziliungana mwaka 1964 na kuunda serikali moja ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya waasisi wetu hayati Mwl Julius Kambarage Nyerere (Baba wa Taifa) na hayati Sheikh Abeid Amani Karume wa Zanzibar, hivyo mpaka leo watanzania wote tunaendelea kuuenzi muungano huu kwa amani na upendo.
Na mwaka huu wa 2018,Tanzania inaadhimisha miaka 54 ya Muungano, ambapo kauli mbiu ya siku ya Muungano kwa mwaka 2018, ni
“Muungano wetu ni fahari yetu, tuuenzi”
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa