Mkuu wa Wilaya ya Newala Newala Mhe. Aziza Mangosongo leo tarehe 20/05/2021 amezindua rasmi zoezi la ugawaji wa dawa za kichocho na minyoo ya tumbo kwa watoto wa shule za msingi zilizopo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Newala kwenye shule ya msingi Chiwonga.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mratibu wa magonjwa yasiyopewa kipaumbele, Dkt. Hamis Mpoteni amesema kuwa zoezi hilo la ugawaji wa dawa za kichocho na minyoo linafanyika katika shule zote za msingi zilizopo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Newala.
"Zoezi hili linafanyika katika shule zote za msingi 76 zilizopo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Newala ikiwa ni muendelezo wa utoaji kinga tiba ambao hutolewa kila mwaka kwa lengo la kuwakinga na kuwatibu watoto na magonjwa ya kichocho na minyoo ya tumbo ambayo hayapewi kipaumbele na jamii licha ya kuwa na athari kubwa kwa watoto hasa upande wa ukuaji wa mwili na akili". Alisema Dkt. Mpoteni.
Dkt. Mpoteni ameeleza kuwa magonjwa hayo ni hatari kwa kuwa yanaweza kusababisha vifo japo yanaweza kuzuilika kwa kuzingatia usafi wa mikono na mwili; usafi wa choo na mazingira; kujiepusha kuoga, kuogelea na kutembea bila viatu kwenye maji yaliyotuama; kutibiwa haraka mara baada ya kuona dalili au kugundulika na magonjwa hayo.
Akizindua zoezi hilo, Mhe. Mangosongo amewataka wazazi kuzingatia usafi kwao na kwa watoto wao na kuwa magonjwa yote yana madhara kama hayajapatiwa tiba na kinga kwa wakati.
"Madhara ya kutozingatia kinga na tiba ya magonjwa ya minyoo ya tumbo na kichocho ni kupata kansa ya kibofu, ugonjwa wa minyoo utakaosababisha madhara kwenye utumbo, kupungukiwa damu mwilini na mama mjamzito kuzaa mtoto mwenye udumavu." Alisema Mhe. Mangosongo.
Aidha wakati huo huo, wakazi wa Chiwonga walipata fursa ya kupewa elimu ya lishe bora na malezi.
Zoezi hilo lilizinduliwa kwa watoto kupatiwa dawa hizo na litaendelea kutolewa katika shule zote za msingi zilizopo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Newala.
Wazazi wa watoto hao walitumia nafasi hiyo kuishukuru Serikali kwa kuwaletea huduma hiyo kwani inasaidia kuwakinga watoto wao na magonjwa hayo.
Uzinduzi huo ulihudhuriwa na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Newala, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Mhe. Isabela Makumbuli, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Bw. Friday Sondasy, Diwani wa kata ya Chiwonga Mhe. Kazumari Nauma, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Dkt. George Matiko, Wakuu wa Idara na Vitengo wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala na wananchi wa kijiji cha Chiwonga.
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa