Viongozi, watendaji na wawezeshaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala, jana tarehe 19/04/2021 wamejengewa uelewa kuhusu utekelezaji wa kipindi cha pili cha TASAF awamu ya tatu kwenye kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa chuo cha ualimu Kitangari.
Bw. Majuto Kayambwa (aliyesimama), mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, akitoa maelezo kuhusu utekelezaji kipindi cha pili cha TASAF awamu ya tatu kwenye kikao kazi cha kujenga uelewa wa pamoja kwa viongozi, wataalamu na wawezeshaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala.
Akitoa maelezo kuhusu kikao kazi hicho, Bw. Majuto Kayambwa, kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF alisema kuwa mafunzo hayo ya kujenga uelewa wa pamoja ni ya kwanza katika utekelezaji wa kipindi cha pili cha TASAF awamu ya tatu.
"Tathmini ya utekelezaji wa kipindi cha kwanza cha TASAF awamu ya tatu inaonyesha kuwa mpango umechangia kwa kiasi kufikia adhma ya Serikali ya kupunguza umasikini nchini, kwa kupunguza umasikini wa mahitaji ya msingi kwa kaya kwa 10%, na umasikini uliokithiri umepungua kwa 12% kwa kaya masikini sana nchini." Alisema Bw. Kayambwa.
Akiendelea kutoa ufafanuzi huo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bw. Kayambwa alisema kuwa pamoja na mafanikio hayo, maeneo yaliyofikiwa katika kipindi cha kwanza cha TASAF awamu ya tatu ni 70% tu ya vijiji vyote nchini, hivyo bado kuna wananchi wanaoishi katika hali duni kwenye maeneo ambayo hayakufikiwa.
"Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeamua kuendelea na kipindi cha pili cha TASAF awamu ya tatu ili kaya zote zinazoishi katika mazingira duni zipate usaidizi wa Serikali kupitia TASAF kwa kuwawezesha kufanya kazi na kupambana na umasikini." Alisema Bw. Kayambwa.
Washiriki wa kikao kazi cha kujenga uelewa wa pamoja kuhusu utekelezaji wa kipindi cha pili cha TASAF awamu ya tatu wakifuatilia mada zilizokuwa zikitolewa katika kikao hicho.
Kipindi cha pili cha TASAF awamu ya tatu kitatekelezwa katika vijiji/mitaa/shehia zote za Tanzania bara na Zanzibar na kinatarajiwa kuzifikia kaya 1,450,000 zenye watu zaidi ya 7,000,000 kote nchini hii ikiwa ni ongezeko la kaya 350,000 ambazo hazikupata fursa hiyo katika utekelezaji wa kipindi cha kwanza cha TASAF awamu ya tatu ambacho kimekamilika.
Utekelezaji wa kipindi cha pili cha TASAF awamu ya tatu utazingatia zaidi kuwezesha kaya zitakazoandikishwa kwenye mpango kufanya kazi ili kuongeza kipato, huduma za jamii kuongezwa na kuboreshwa ili kutoa uhakika wa lishe bora kwa kaya husika pamoja na huduma bora za elimu na afya.
Walengwa wa mpango huu ni zile kaya duni zinazoishi katika vijiji/mitaa/shehia ambazo zina watoto chini ya miaka mitano wanaohudhuria kliniki; wanafunzi wanaosoma shule za awali, msingi na sekondari; mama wajawazito pamoja na walemavu.
Kaya hizo zitakazoingia kwenye kipindi cha pili cha TASAF awamu ya tatu zutanufaika kwa kupewa ruzuku za msingi (kwa kaya iliyoandikishwa kwenye mpango); ruzuku ya kutimiza masharti ( kwa kaya iliyoandikishwa kwenye mpango yenye watoto wa kuhudhuria kliniki au shule) ruzuku ya ulemavu ( kwenye kaya iliyoandikishwa kwenye mpango yenye mtu mwenye ulemavu) na ruzuku ya watoto chini ya miaka 18 wanaoishi kwenye kaya husika. Hata hivyo mpango huu unatoa ajira kwa kaya masikini zenye watu wenye uwezo wa kufanya kazi hususani katika kipindi cha ari.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Mhe. Tamimu Ladda akizungumza katika kikao kazi cha kujenga uelewa wa pamoja kuhusu utekelezaji wa kipindi cha pili cha TASAF awamu ya tatu
"Sisi kama viongozi na wataalamu tuna wajibu wa kusimamia vizuri mpango huu ili kuhakikisha kaya zitazotambuliwa na kuandikishwa zinanufaika na mpango huu, tukafanye kazi hii kwa uadilifu ili kufikia malengo ya Serikali kupitia kipindi cha pili cha TASAF awamu ya tatu ya kupunguza umasikini na kuchochea ukuaji wa uchumi ukiwemo ule wa viwanda ambao nia ajenda muhimu ya Serikali." Alisema Mhe. Tamimu Ladda, mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bw. Duncan Thebas, alisisitiza jambo katika kikao kazi cha kujenga uelewa wa pamoja kuhusu utekelezaji wa kipindi cha pili cha TASAF awamu ya tatu kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa chuo cha ualimu Kitangari, Wilaya ya Newala.
Pia Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Bw. Duncan Thebas amewataka viongozi wa maeneo ambayo kaya hizo zitatambuliwa kutoa ushirikiano kwa wawezeshaji watakaoenda kusimamia zoezi hilo ili kaya zote zenye sifa ziingie kwenye kipindi cha pili cha TASAF awamu ya tatu.
Sehemu ya pili ya mpango wa TASAF awamu ya tatu ilizinduliwa tarehe 17/02/2020 jijini Dar es Salaam na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania awamu ya tano, Hayati Dkt. John Magufuli, na kwa Halmashauri ya Wilaya ya Newala umeanza rasmi kwa viongozi na wataalamu kupata uelewa pamoja na wawezeshaji kupewa mafunzo yatakayowawezesha kwenda kuzitambua kaya masikini zilizopo katika eneo lao la utekelezaji.
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa