Mkuu wa Wilaya ya Newala Mhe. Aziza Mangosongo jana siku ya Jumatatu tarehe 24/08/2020 amefanya mkutano wa hadhara na wananchi wa kijiji cha Chilondolo kata ya Mtopwa, Halmashauri ya Wilaya ya Newala.
Mkutano huo ni muendelezo wa ziara za Mhe. Mangosongo katika vijiji vya Newala ili kusikiliza na kutatua kero za wananchi na aliwataka wakazi wa Chilondolo kutoa kero walizonazo ili azifanyie kazi kwa maendeleo ya Newala.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika mkutano huo, wakazi wa Chilondolo wamemueleza Mhe. Mangosongo juu ya uchakavu wa miundombinu ya majengo ya shule ya msingi Mtopwa; ubovu wa barabara ya kutoka Mtopwa kupitia Chilondolo hadi Tulieni; kukosekana kwa zahanati katika kijiji chao na kufanya wakazi wa hapo kupata huduma za afya katika kijiji cha Mnyeu ambapo ni mbali kutoka katika makazi yao; uchache wa virura vya kuchotea maji; upewaji wa kipaumbele kwenye matibabu kwa wazee; upatikanaji wa vitambulisho vya Taifa na kutaka Serikali iwasaidie kutatua kero hizo.
Aidha kutokana na hoja hizo, Mhe. Mangosongo aliwaruhusu wataalam wanaohusika na sekta zenye hoja hizo kutoa ufafanuzi na majibu kwa wananchi na baadaye alitoa maelekezo kwa wataalamu hao kwa ajili ya utekelezaji.
Mhe. Mangosongo kwa upande wa miundombinu ya majengo yakiwemo ya shule na zahanati, aliwataka wakazi wa Chilondolo kuanza ujenzi wa miundombinu hiyo kwa nguvu zao wenyewe na baadaye Serikali itawasaidia kumalizia baada ya wao kufikia hatua ya lenta katika ujenzi huo. Aidha, kuhusu miundombinu ya matundu manne ya vyoo ambavyo vimeshaanza kujengwa kwa nguvu za wananchi, Mhe. Mangosongo ameahidi kuwapatia vifaa katika ujenzi huo baada ya kufikia vigezo vinavyotakiwa vya mradi wa shule ni choo.
Kwa upande wa ukarabati wa barabara, Mhe. Mangosongo amewataka wakala wa barabara vijijini (TARURA) kuanza uchongaji wa barabara hiyo mara moja kwa kuwa wamemuahidi kuwa imewekwa kwenye mpango wa matengenezo ya mwaka huu wa fedha 2020/2021, pia wataalamu wa wakala wa maji vijijini (RUWASA) kufika kijijini hapo ndani ya wiki hii kufanya tathmini ya namna ya kuongeza vilula vya kuchotea maji.
Kwa upande wa vitambulisho vya Taifa, wananchi wa Chilondolo wametakiwa kuwasilisha taarifa sahihi NIDA pale yanapohitajika marekebisho ili kuondoa tatizo la taarifa zao kutoshabihiana na kupelekea vitambulisho vyao kutopataikana kwa wakati.
Pia, Mhe. Mangosongo ameitaka idara ya afya kuhakikisha wamemuweka muhudumu atakayewapa maelekezo wazee pindi wanapofika kupata huduma za afya ili wapate huduma hiyo kwa haraka.
Mhe. Mangosongo katika mkutano huo aliongozana na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Bi. Magreth Likonda na wakuu wa Idara na Vitengo wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala.
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa