Pichani ni Mkuuwa Wilaya ya Newala Mhe. Aziza Mangosongo (wa pili kutoka kushoto waliokaa) akitia saini mkataba wa lishe katika tathmini ya Afua ya Lishe iliyofanyika tarehe 10/09/2018 katika ukumbi wa Boma Mkoani Mtwara.
Mkuu wa Wilaya ya Newala Mhe. Aziza Mangosongo, ametia saini mkataba wa utekelezaji wa mpango wa Afua za Lishe unaotekelezwa kwa awamu nyingine Wilayani Newala.
Hatua hiyo imefikia wakati wa kikao maalum cha tathmini ya Afua ya Lishe kilichofanyika tarehe 10/09/2018 katika ukumbi wa Boma Mkoani Mtwara ambapo Mkoa ulibaini mapungufu na changamoto mbalimbali zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa mpango huo kwa mwaka 2017/2018 ikiwa ni pamoja na utafiti wa kidemografia wa Afya wa mwaka 2015/2016 ulioonyesha kupungua kwa udumavu kutoka asilimia 44 hadi asilimia 38, ingawa pamoja na kupungua kwa viwango hivyo, inakadiriwa kuwa bado kuna zaidi ya watoto elfu 78 na mia 8 na 7 (78,807) waliopo Mkoani Mtwara wamedumaa na hasa watoto wadogo pamoja na wamama wajawazito ambao wameonekana kutozingatia taratibu za lishe wakati wa ujauzito na pindi wanapojifungua, hali inayopelekea wao wenyewe pamoja na watoto wengi kupata utapiamlo na hivyo kupunguza nguvu kazi ya Taifa inayokusudiwa kuwepo katika nchi yetu ya Tanzania ya Viwanda.
Kufuatia hali hiyo Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Gelasius Byakanwa, ameingia mkataba maalum na Wakuu wa Wilaya zote za Mkoa wa Mtwara ikiwemo Wilaya ya Newala, ambao nao wataingia mkataba na wakurugenzi wao wa Halmashauri za Miji na za Wilaya, ili kuhakikisha kila Wilaya kwa ujumla inatekeleza mpango wa Lishe bora kwa jamii na kuondokana na tatizo la udumavu wa akili, utapiamlo na magonjwa yatokanayo na hiyo hali katika jamii zetu.
Nae Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Dr.Wedson Sichalwe ameziagiza Halmashauri zote za Mkoa wa Mtwara kuhakikisha zinatenga fedha kulingana na idadi ya watoto waliopo katika Halmashauri ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanawashirikisha wadau mbalimbali pamoja na viongozi wa dini kusaidia kutoa elimu ya mambo ya Lishe ili jamii iondokane na imani potofu juu ya mambo ya uzazi na lishe kwani wanavyohusisha madini ya Folic Acid na madini ya chuma sivyo ilivyo.
Mkataba wa utekelezaji wa mpango wa lishe Wilayani Newala unatarajiwa kumaliza ama kupunguza tatizo kubwa la udumavu wa akili na utapiamlo kwa wamama na watoto Wilayani Newala.
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa