Mkuu wa mkoa wa Mtwara Mhe. Gelasius Gasper Byakanwa amesitisha kampeni zote zinazoendelea za kuvunja au kutovunjwa kwa chama kikuu cha Ushirika TANECU, mpaka Mkoa utakapokuwa umepata muongozo wa Mrajisi.
Mhe. Byakanwa ameyasema hayo leo tarehe 25/05/2018 alipokuwa kwenye kikao maalum na viongozi wa vyama vya ushirika vya Newala na Tandahimba, kamati za ulinzi na usalama za Wilaya za Newala na Tandahimba, viongozi wa TANECU, wakurugenzi pamoja na wenyeviti wa Halmashauri za Newala na Tandahimba, kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala.
Kutokana ushirika kutengeneza kundi la watu ambao walibahatika kuwa wanachama wa ushirika, na hadi sasa ndio wanaotambulika kama wanachama wa ushirika, Mhe. Byakanwa ameishauri Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, pamoja na Mrajisi, kwamba kwa sasa sheria ya ushirika imtake kila mkulima kuwa mwanachama wa ushirika ili kuongeza wigo wa wanachama na kuwapata watu ambao wana sifa na wanaoweza kuleta mabadiliko ndani ya ushirika, kwani kuendelea kuvunja ushirika na kuwaacha wanachama wale wale, hakutaleta mabadiliko bali kutakuwa kunakidhi haja za watu wale wale tu.
Aidha Mhe. Byakanwa ambaye ndiyo kiongozi wa Mkoa wa Mtwara, amesema kama itaonekana ushauri huo haufai, basi Mrajisi aje na Muongozo kamili, ila kwa kuwa hadi sasa bado muongozo huo haujatoka, ni marufuku kwa mtu yoyote kuendelea na kampeni ya kutaka kuvunja au kutovunjwa kwa chama kikuu cha ushirika TANECU, kwani Wizara ya Kilimo ni sikivu, na Mrajisi ni msikivu, na kama serikali ina nia njema ya kuimarisha ushirika, iunde tume ili kuchuchunguza nani kafanya nini, ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua wale wote waliohusika, na kama itabidi kuivunja TANECU, basi uwekwe utaratibu mzuri wa kuvunja ambao hautaleta madhara kwa wakulima.
Mhe. Byakanwa ameongeza kuwa, kwa kuwa mpaka sasa hakuna muongozo wowote wa Serikali kuhusiana na kuvunjwa kwa TANECU, kila kitu kinachoendelea na mikakati inayopangwa na baadhi ya wanasiasa na wanaushirika, imesitishwa rasmi, hivyo wabunge na wanasiasa wote wasijihusishe na swala hilo, kwani kujihusisha na swala hilo kunaweza kuwa chanzo cha kuvunjika kwa ushirika wa wakulima.
Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara amesema serikali imetoa msimamo na muongozo kuhusiana na bei ya Sulpher ambayo ni shilingi 32,000/= tu, na hivyo hairuhusiwi kuuzwa kwa bei ya zaidi ya shilingi 32,000/=, na amewaagiza wakuu wa Wilaya husika, kusimamia na kuwachukulia hatua wale wote watakaobainika kuuza sulpher hiyo kwa bei ya zaidi ya sh. 32,000/=.
Maamuzi ya kusitisha kampeni za kuvunja au kutovunjwa kwa chama kikuu cha ushirika TANECU, yamekuja muda mfupi baada ya serikali kupitia Bunge, kutangaza kuvunja chama hicho kikuu cha ushirika cha Newala na Tandahimba (TANECU).
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa