Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Joseph Magufuli amefanya ziara ya siku moja Wilaya ya Newala siku ya Jumatano tarehe 03/04/2019.
Ziara hiyo ilihusisha kuwasalimia wananchi wa Newala na kuweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa kuboresha miundombinu ya chuo cha ualimu Kitangari.
Akimkaribisha Mhe. Rais Magufuli katika chuo cha ualimu kitangari, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Ndalichako alieleza kuwa chuo hicho kilianza rasmi mwaka 1937 kama shule na mwaka 1975 kilibadilishwa na kuwa chuo cha ualimu.
Mradi huo wa ujenzi wa kuboresha miundombinu ya chuo ulianza mwezi Julai 2016 na unahusisha ujenzi wa kumbi za mihadhara, mabweni ya wanafunzi, maabara, madarasa, ofisi na visima vya maji. Mradi huo unagharimu jumla ya shilingi bilioni nane na milioni mia mbili na sitini na tisa ambapo fedha za mradi huo zimetolewa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Canada.
Akizungumza na wakazi wa Newala, Mhe. Rais Magufuli alianza kwa kuwashukuru wana Newala kwa kumpa kura za kutosha kumfanya awe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na aliwahakikishiwa kuwa atawalipa kwa kuwafanyia kazi.
Pia Mhe. Rais Magufuli aliishukuru Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kumualika kuja kuweka jiwe la msingi katika chuo cha ualimu Kitangari ikiwa ni utekelezaji wa ahadi alizozitoa za kuendeleza elimu ikiwa ni pamoja na kutoa elimu bure, mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu, kuboresha miundimbinu ya shule na kukarabati na kuendeleza miundombinu ya vyuo vya ualimu.
Akiendelea kuzungumza na wakazi wa Newala, Mhe. Rais Magufuli alitumia nafasi hiyo kuishukuru Serikali ya Canada kwa michango yao katika sekta mbalimbali nchini Tanzania ikiwemo elimu na pia amewaomba wananchi wa Newala kuutunza mradi huo ili udumu.
Mhe. Rais Magufuli pia amewaeleza wana Newala kuwa Serikali imedhamiria kupambana na dhuluma hasa kwa wakulima wa kipato cha chini kwa kuzuia kangomba na kuamua kununua korosho kwa shilingi 3300 na mpaka sasa asilimia 90 ya wakulima wameshalipwa na waliobaki wanaendelea kulipwa. Amesisitiza kuwa lengo la Serikali la kupeleka fedha moja kwa moja kwa wakulima ni kuboresha maisha yao.
Wakati huohuo Mhe. Rais Magufuli amewasamehe wananchi wote walionunua korosho kwa kangomba na amewaahidi wote walionunua korosho kwa kangomba watalipwa fedha zao kulingana na kiasi cha korosho walichouza kwa masharti ya kuomba msamaha kwa kuandika barua na kuahidi kutorudia tena kununua kangomba.
Pia aliahidi barabara ya kutoka Mtwara mpaka Newala itatengenezwa kwa lami kwa kilomita 100 kuanzia Mnevata hadi Newala na aliwapongeza wana Newala kwa kufanya vizuri katika kilimo na kukuza uchumi wa Wilaya na aliwataka kuendelea kuiamini Serikali na kufanya kazi kwa bidii na maendeleo yatapatikana.
Ziara ya Mhe. Rais Magufuli katika Wilaya ya Newala ilikuwa ya siku moja na aliongozana na viongozi mbalimbali wakiwemo Balozi wa Canada nchini Tanzania Mhe.Pamela O’Donnell, Mawaziri wa wizara mbalimbali, Wabunge, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, wakuu wa Wilaya na wakurugenzi wa Halmashauri.
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa