Kampeni ya kusajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano ambao hawajapata vyeti vya kuzaliwa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Newala imezinduliwa leo tarehe 21/06/2021.
Kampeni hiyo imehusisha mafunzo ya siku moja kwa wasajili ngazi ya kata na vijiji, na usajili na utoaji wa vyeti kwa watoto chini ya miaka mitano kwa siku nne mfululizo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Bw. Duncan Thebas, akifungua mafunzo ya wasajili kuelekea kampeni ya usajili na utoaji wa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano.
Akifungua mafunzo maalum kwa wasajili wa zoezi hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Bw. Duncan Thebas amewataka wasajili hao kufanya kazi kwa uadilifu kwa kuwatambua watoto wote wenye umri chini ya miaka mitano, wanaotakiwa kupata vyeti vya kuzaliwa ili wapate.
"Moja ya ulinzi wa mama na mtoto ni takwimu za mtoto wake mwenyewe, hivyo tukachukue takwimu zote za watoto ambazo zipo katika maeneo yetu." Alisema Ndg. Thebas
Dhumuni kuu la kuanza na mafunzo hayo ni kukumbushana majukumu ya wasajili hao na kujua changamoto wanazokumbana nazo katika kazi hiyo na kutafutia ufumbuzi wa pamoja ili kuleta ufanisi zaidi katika kampeni hiyo.
Mwezeshaji kutoka Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) makao makuu Bw. Baraka Mollel, akitoa maelekezo kwa wasajili namna ya kujaza rejista ya taarifa za mtoto anayetakiwa kutengenezewa cheti cha kuzaliwa.
Akiwezesha mafunzo hayo, Bw. Baraka Mollel kutoka Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) makao makuu ameeleza kuwa RITA, UNICEF na Ubalozi wa CANADA walianzisha mfumo wa usajili wa watoto chini ya miaka mitano kwa kuwa kundi hilo la watoto ni muhimu na ni kiashiria muhimu katika mpango wa maendeleo endelevu.
"Katika siku hizi za kampeni, mtoto mwenye umri chini ya miaka mitano anaweza kusajiliwa sehemu yoyote katika ardhi ya Tanzania. Aidha baada ya kampeni hii, watoto wanatakiwa kusajiliwa katika eneo la Halmashauri husika waliyozaliwa na ambao wapo ndani ya siku 90 baada ya kuzaliwa, waliozidi siku 90 watatakiwa kusajiliwa katika ofisi za wakuu wa Wilaya." Alisema Bw. Mollel.
Washiriki wa mafunzo ya usajili na utoaji wa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano wakifuatilia mafunzo ya ujazaji rejesta za taarifa za watoto kwa vitendo.
Kampeni hii ya siku tano inahusisha siku moja ya kikao kazi na siku nne za kusajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano.
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa