Kamati za ulinzi na usalama wa mwanamke na mtoto kutoka katika kata za Halmashauri ya Wilaya ya Newala zajengewa uwezo wa kutekeleza majukumu yao leo tarehe 22/06/2021 kwa kupitia kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa chuo cha walimu Kitangari.
Majukumu ya kamati hizo za ulinzi wa mama na mtoto ni kusimamia mpango kazi wa kijiji na kata na kuandaa taarifa zote za utekelezaji wa mpango; kutambua na kusajili watoto wote wanaoishi katika mazingira hatarishi; na kutoa taarifa kwenye mamlaka husika iwapo yatatokea maswala ya kikatili yanayofanywa kwa wanawake na watoto.
Akifungua kikao kazi hicho, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Bi. Magreth Likonda amewataka washiriki wote kuzingatia maelekezo watakayopewa kwa kuwa wao ni watu muhimu sana katika usimamizi wa haki za wanawake na watoto kwa kuwa ni miongoni mwa jamii hiyo.
"Nyinyi kama wawakilishi wa jamii, mmepewa dhamana ya kusimamia ulinzi na usalama wa mwanamke na mtoto, mkahakikishe mnatekeleza majukumu yenu vyema kwa kuibua na kukemea viashiria vyote vya ukatili huo katika jamii". Alisema Bi. Likonda.
Kamati hizi zipo katika ngazi ya Taifa, Mkoa, Halmashauri, Kata na Kijiji zenye jukumu la kutokomeza maswala yote yanayohusu ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Aidha, baada ya kikao kazi hicho, wajumbe wa kamati hiyo watakuwa na zoezi la kuwatambua watoto wenye mahitaji maalum katika mazingira wanayotoka kwa kuwa jamii kwa ujumla ina jukumu la kuhakikisha mtoto analindwa na anaishi katika mazingira salama.
Mratibu wa Mpango wa Kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto (MTAKUWA) Newala Bw. Bakari Mnali, akitoa mafunzo kwa wajumbe wa MTAKUWA ngazi ya Kata.
"Hii iwe chachu ya Watendaji wa Kata na Vijiji ambao ndiyo wasimamizi wa MTAKUWA katika maeneo yenu, kuona namna shughuli za Ustawi wa jamii zinaingia katika utekelezaji wa shughuli zao za kila siku na taarifa zake ziwe zinaingia katika taarifa za vijiji za kila mwezi na taarifa za kata za kila baada ya miezi mitatu." Alisema Bw. Mnali, Mratibu wa Mpango wa Kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto (MTAKUWA) Halmashauri ya Wilaya ya Newala.
Kikao kazi hicho ni cha siku tatu, kuanzia tarehe 22 hadi 24/06/2021.
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa