Wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama wa mwanamke na mtoto wamepatiwa mafunzo juu ya majukumu yao katika ulinzi na usalama wa mwanamke na mtoto.
Mafunzo hayo yaliyoanza tarehe 08/06/2021 yalihusu utekelezaji wa kuimarisha uchumi wa kaya; mila na desturi za jamii; mazingira salama ya mwanamke na mtoto; malezi bora, kuimarisha mahusiano katika kaya na kuziwezesha familia juu ya haki na wajibu wa mtoto; utekelezaji na usimamizi wa sheria za mtoto; huduma kwa waathirika wa ukatili na mazingira salama shuleni na stadi za maisha.
Malengo ya mafunzo hayo ni kuiwezesha kamati ya ulinzi na usalama wa mwanamke na mtoto kutekeleza vyema Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza ukatili dhidi ya wanawakena watoto (MTAKUWA) ambao unalenga kusimamia haki na maendeleo ya mtoto na kuzuia ukatili dhidi ya mwanamke na mtoto na kuhakikisha wanapata haki zao na kutimiza wajibu wao vyema.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo, Mratibu wa MTAKUWA wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Bw. Bakari Mnali, amesema kuwa mafunzo hayo ni muhimu sana kwa kuwa yanaiwezesha kamati ya MTAKUWA kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
"Mafunzo haya yanawawezesha wajumbe wa kamati ya MTAKUWA kujua majukumu yao na namna watakavyofanya kazi katika swala zima la ulinzi na usalama wa mwanamke na mtoto." Alisema Bw. Mnali.
Akifunga mafunzo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala, Bi. Lucy Matem ambaye ni Mwanasheria wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala, amewataka wajumbe hao kutimiza wajibu wao na kuzingatia yale yote waliyofundishwa ili kutimiza adhma ya ulinzi na usalama wa wanawake na watoto.
Mafunzo hayo yamefanyika kwa siku tano na yaliwahusisha wajumbe wa MTAKUWA wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala wakiwemo wataalam, wawakilishi wa watu wenye ulemavu, wawakilishi wa vikundi vya maendeleo ya wanawake na viongozi wa dini ambao ni wajumbe wa MTAKUWA kulingana na muongozo wake.
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa