Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Newala leo Alhamisi tarehe 4/2/2021 imefanya ziara ya kufuatilia utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) katika Halmashauri ya Wilaya ya Newala kwa kutembelea miradi minne ya maendeleo inayotekelezwa katika Halmashauri.
Kamati hiyo ikiongozwa na mwenyekiti wa CCM wilaya ya Newala Bw. Jabir Mtanda, imefanikiwa kutembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa barabara ya Mkwiti-Lochinu-Nyangao ambapo kipande cha urefu wa Km 3.5 kitatengenezwa ili kufungua mawasiliano katika kijiji cha Lochinu na Nyangao.
Akiwasilisha taarifa ya mradi kwa kamati hiyo, mhandisi wa TARURA Halmashauri ya Wilaya ya Newala Bw. Sylvester Balama ameeleza kuwa katika kuhakikisha barabara hiyo inapitika, kwa mwaka wa fedha 2020/2021 Serikali imetenga jumla ya Tsh.90,864,750.00.
"utengenezaji wa barabara hii utahusisha matengenezo ya kawaida, matengenezo ya sehemu korofi, matengenezo ya muda maalum, ujenzi wa boksi kalavati moja na kalavati la kawaida moja." Alisema mhandisi Balama.
Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Newala ikipokea maelezo ya mradi wa ujenzi wa madarasa mawili na ofisi moja katika shule ya sekondari Mpotola
Wakiendelea na ziara hiyo, kamati ya siasa ya Wilaya ya Newala pia ilifanikiwa kukagua mradi wa ujenzi wa madarasa mawili na ofisi moja katika shule ya sekondari Mpotola wenye thamani ya Tsh. 40,000,000 ambao umekamilika; mradi wa usambazaji wa umeme katika kijiji cha Mchemo; na mradi wa ujenzi wa majengo ya maabara na mapokezi ya wagonjwa wa nje (OPD) katika hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Newala.
Aidha Mhe. Mtanda ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Newala kwa utekelezaji mzuri wa miradi ya maendeleo na kusisitiza fedha zote zinazoletwa na Serikali zitumike vizuri kama ilivyoelekezwa na miradi ikamilike kwa wakati.
"Nimekagua miradi yote minne na nimeridhika kuwa thamani ya fedha na namna miradi inavyotekelezwa vinalingana." Amesema Mhe. Mtanda.
Kamati hiyo ya siasa ya Wilaya ya Newala imefanya ziara hiyo ikiwa ni moja ya shughuli zilizofanywa katika kuadhimisha miaka 44 ya kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi (CCM).
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa