Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Marco Gaguti amewataka madiwani na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala kubadilika katika usimamizi wa ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kufikia malengo ya Halmashauri.
Mhe. Gaguti ameyasema hayo leo tarehe 16/06/2020 alipohudhuria mkutano wa baraza maalum la madiwani la kupitia taarifa ya majibu ya hoja za Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2019/2020 lililofanyika katika ukumbi wa mikutano wa chuo cha walimu Kitangari.
"Waheshimiwa madiwani msimamie mapato katika maeneo yenu kwa kuwa vyanzo vya mapato vipo huko mlipo.........Mkoa wa Mtwara nataka uwe ni mkoa kinara kwenye kukusanya mapato" alisema Mhe. Gaguti.
"Halmashauri hii ni lazima ikusanye mapato yake kwa asilimia mia moja, na kama kuna watendaji ambao wanaihujumu hii Halmashauri nitachukua hatua stahiki" amesema Mhe. Gaguti.
Akizungumza katika mkutano huo wa baraza maalum la madiwani, Mhe. Gaguti amewataka watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala kuwa wabunifu wa vyanzo vya mapato ambavyo vitaiwezesha Halmashauri kukusanya kwa asilimia mia moja na kuzitumia fedha hizo vizuri kwa maendeleo yao.
"Lazima tuwe wabunifu wa kutafuta vyanzo vipya vya mapato na pia kuwe na matumizi sahihi ya fedha zitakazokusanywa. Halmashauri mhakikishe mnapeleka fedha asilimia ishirini za vijiji ili fedha hizo zikatumike kufanya shughuli mbalimbali katika ngazi ya vijiji na kusababisha uchumi wa Halmashauri kukua." Alisema Mhe. Gaguti.
Aidha washiriki wa mkutano huo walijulishwa na Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Newala kwa hesabu za mwaka wa fedha 2019/2020 imepata hati safi, kulikuwa na hoja therathini na baada ya uhakiki hoja kumi na nane zilifungwa na hoja kumi na mbili hazijafungwa zinaendelea kufanyiwa kazi.
"Halmashauri ya Wilaya ya Newala ilifanyiwa ukaguzi wa hesabu na Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha unaoishia tarehe 30 Juni, 2020. Kwa hesabu za mwaka wa fedha 2019/2020, Halmashauri ya Wilaya ya Newala ilipata hati safi, kwa niaba ya ofisi ya taifa ya ukaguzi wa hesabu za Serikali napenda kuwapongeza Halmashauri ya Wilaya ya Newala kwa kupata hati safi." Alisema Bw. Fastek Mwampashe kwa niaba ya Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali.
Wakati huo huo, katika kudumisha utawala bora, Mhe. Gaguti amewaagiza madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala kwenda kushughulikia kero za wananchi katika maeneo yao.
"Hii ndiyo kazi tuliyoomba, hivyo niwaombe waheshimiwa madiwani muwe na siku nyingi za kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi". Alisema Mhe. Gaguti.
Baraza hilo maalum la madiwani limejadili majibu ya hoja za Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali na kuitaka menejimenti ya Halmashauri ya Wilaya ya Newala kufanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa na CAG, kamati ya fedha, utawala na mipango ili hoja zilizobaki ziweze kufungwa.
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa