Mkuu wa Wilaya ya Newala Bi. Aziza Mangosongo siku ya Ijumaa tarehe 15 Februari 2019 amezindua rasmi zoezi la upandaji wa miti Wilaya ya Newala kwa mwaka huu 2019 katika eneo la shule ya msingi Mtunguru iliyopo kata ya Mtunguru Wilaya ya Newala.
Mkuu wa Wilaya ya Newala Bi. Aziza Mangosongo (aliyesimama) akizungumza na waliohudhuria kwenye uzinduzi wa upandaji wa miti kiwilaya.
Upandaji huo wa miti ni njia ya kutunza mazingira ikiwa ni pamoja na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi yanayosababishwa hasa na ukataji wa miti unaopelekea kukosekana kwa mvua za kutosha hivyo kuathiri shughuli za kilimo ambacho ni tegemeo kubwa kwa wananchi wa Newala.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Bw. Mussa Chimae akishiriki kupanda mti na mwanafunzi wa darasa la awali shule ya msingi Mtunguru
Akizungumza baada ya zoezi la upandaji wa miti hiyo, Afisa Misitu mwandamizi wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Bw. Lukumbwiso Mbwilo ameeleza kuwa jumla ya miti 960 imepandwa kwa siku hiyo ambayo inajumuisha miti ya mbao, matunda pamoja na mikorosho. Aidha zoezi hilo ni endelevu katika maeneo yote ya Wilaya ya Newala kwa kuwa Wilaya inatakiwa kupanda miti 1,500,000 na Halmashauri ya Wilaya ya Newala pekee inatakiwa kupanda miti 750,000 katika maeneo yake mbalimbali.
Uzinduzi huo ulihudhuriwa na kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Newala, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Bw. Mussa Chimae, wakuu wa idara na vitengo wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala, viongozi wa chama cha mapinduzi CCM, meneja wa benki ya NMB Newala, meneja wa wakala wa misitu Wilaya ya Newala, waheshimiwa madiwani, na wananchi wa kata ya Mtunguru.
Diwani wa kata ya Mtunguru Mhe. Chitwanga Ndembo akishiriki kupanda mti katika eneo la shule ya msingi Mtunguru.
Zoezi la upandaji wa miti ni agizo la Serikali ambapo kila mwaka ni lazima kuwe na siku maalum ya kupanda miti. Kwa mwaka huu 2019 kitaifa zoezi hili litazinduliwa rasmi tarehe 01 Aprili 2019 ila kwa kuwa mwezi Aprili msimu wa mvua kwa Wilaya ya Newala utakuwa unafikia mwisho ndiyo maana uzinduzi kiwilaya umefanyika rasmi mwezi huu Februari.
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa