Bodi ya taasisi ya maendeleo Newala NDF leo imekabidhi rasmi shule ya sekondari kitangari NDF kwa Chuo cha mafunzo ya ufundi stadi VETA Tanzania.
Makabidhiano hayo ya majengo na eneo la shule yamefanyika baina ya mwenyekiti wa NDF Mhe. Chitwanga Ndembo na Kaimu Mkurugenzi wa VETA Tanzania Mhandisi Joseph Mwanda na yameshuhudiwa na wajumbe wa bodi ya NDF, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Bw. Mussa Chimae, mbunge wa Newala mjini Mhe. George Mkuchika, waheshimiwa madiwani, wenyeviti wa serikali za vijiji vya kitangari Hospitali na kitangari sokoni na viongozi wa dini.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, mheshimiwa Ndembo alisema kuwa dhumuni kubwa la kuanzisha chuo hicho cha VETA ni kuwawezesha vijana wa Newala na Tanzania kwa ujumla kupata elimu ya ufundi stadi hivyo kwenda sambamba na kauli mbiu ya Serikali ya kuijenga Tanzania ya Viwanda.
Mwenyekiti wa bodi ya taasisi ya maendeleo Newala Mhe. Chitwanga Ndembo (aliyesimama) akizungumza wakati akikabidhi majengo ya Sekondari ya kitangari NDF kwa VETA Tanzania
Aidha, wanafunzi ambao bado wapo katika shule hiyo wataendelea kusoma katika kipindi hiki cha mwaka mmoja wakati VETA wanakarabati majengo hayo ya shule ili yafanane na mazingira ya chuo cha ufundi stadi na baadaye wanafunzi hao watahamishiwa katika shule nyingine.
Kwa upande wake, kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA Tanzania amesema kuwa ni faraja kubwa sana wao kuanzisha chuo Newala na wameshaleta fedha kiasi cha shilingi milioni mia mbili na ishirini na mbili kwa ajili ya ukarabati wa awali wa majengo hayo na mafunzo yataanza rasmi mwezi wa sita mwaka huu kwa kuanzisha kozi mbili za ufundi.
Kaimu Mkurugenzi wa VETA Tanzania mhandisi Joseph Mwanda (aliyesimama) akieleza matarajio ya VETA Tanzania kwa uanzishaji wa chuo hicho Kitangari, Halmashauri ya Wilaya ya Newala.
Uanzishwaji wa chuo hicho ni fursa kwa wakazi wa Newala kwa kuwa vijana watapata nafasi ya kusoma, wananchi watakuwa na fursa ya kupata ajira mbalimbali katika chuo hivyo kukuza ujuzi na uchumi wa wananchi wa Newala na Mkoa wa Mtwara kwa ujumla.
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa