Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Newala limepitisha rasimu ya bajeti ya Tsh. 24,301,601,003.83 kwa mwaka 2018/2019 katika mkutano wa baraza la madiwani uliofanyika siku ya Jumatano tarehe 28/02/2018 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala.
Akiwasilisha rasimu hiyo ya bajeti ya mwaka 2018/2019, Mweka Hazina wa Halmashauri ya wilaya ya Newala Bw. Innocent Magayane, alisema kuwa bajeti hiyo ni kutoka vyanzo mbalimbali vya mapato ikiwemo ruzuku kutoka Serikali Kuu (ikihusisha Tsh. 16,840,956,958.83 ya mishahara; Tsh. 848,015,000.00 matumizi ya kawaida na Tsh.1,791,448,084.00 miradi ya maendeleo), wahisani wa maendeleo Tsh. 3,030,090,961.00 na mapato ya ndani ya Halmashauri Tsh. 1,791,090,000.
Aidha kiasi hicho cha fedha kitatumika katika kuhudumia sehemu kuu tatu ambazo ni mishahara ya watumishi Tsh. 16,840,956,958.83, matumizi ya kawaida ya ofisi za Halmashauri Tsh. 1,850,322,000.00 na kugharamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo Tsh. 5,610,322,045.00.
Akizungumza katika mkutano huo wa baraza la madiwani, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Mhe. Chitwanga Rashid Ndembo aliwasisitiza watumishi na madiwani juu ya kusimamia vizuri ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kuwa ndiyo yanayowezesha kuendesha shughuli za kawaida za Halmashauri.
Mkutano huo ulikuwa wa siku moja kwa ajili ya kujadili na kupitisha rasimu ya mpango na bajeti kwa mwaka 2018/2019 na mpango wa motisha wa watumishi wa Halmashauri kwa mwaka 2018/2019.
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa