Wanawake wa Wilaya ya Newala waadhimisha siku ya mwanamke duniani tarehe 8 mwezi Machi kwa kuwatembelea na kuwafariji wagonjwa katika kituo cha afya Kitangari.
Katika maadhimisho hayo mgeni rasmi alikuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Newala Ndugu. Daniel Zenda ambaye alimuwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Newala Bi. Aziza Mangosongo.
Ndugu. Zenda akimjulia na kumpatia mahitaji mmoja wa wagonjwa waliolazwa katika kituo cha afya Kitangari, Halmashauri ya Wilaya ya Newala.
Ndugu. Zenda aliwaongoza wanawake wa Newala kuwatembelea na kuwafariji wagonjwa ambapo wagonjwa hao walipewa mahitaji mbalimbali yakiwemo sabuni za kuongea na kufulia, maji ya kunywa pamoja na juisi. Pia kituo cha afya kilipatiwa sabuni kwa ajili ya kufanyia usafi.
Akizungumza na wananchi wa Kitangari na wanawake wa Newala kwa ujumla baada ya zoezi la kuwafariji wagonjwa, Ndugu. Zenda ameahidi kuwatafutia ufumbuzi wa upatikanaji wa masoko ya bidhaa za wajasiriamali wa Newala pia amewataka wanawake kuthubutu na kutochagua kazi.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Newala Ndugu. Daniel Zenda (aliyesimama) akizungumza na hadhara iliyojitokeza kwenye maadhimisho ya siku ya mwanamke duniani kata ya Kitangari, Halmashauri ya Wilaya ya Newala.
Akiendelea kuzungumza, Zenda amezipongeza Halmashauri zilizopo Wilaya ya Newala kwa kujitahidi kutoa mikopo kwa vikundi vya wanawake hivyo kuwafanya kuwajibika na amezisisitiza Halmashauri kuendelea kutoa mikopo hiyo kwa vikundi vingi zaidi.
Ndugu. Zenda akikagua bidhaa za biashara za wajasiriamali wa Newala kwenye maadhimisho ya siku ya mwanamke duniani.
Maadhimisho hayo yaliambatana na maonesho ya shughuli mbalimbali zinazofanywa na vikundi vya wanawake wajasiriamali; maonesho ya sanaa za ngoma za asili, muziki wa kizazi kipya, maigizo na michezo mbalimbali ikiwemo kukimbia na vijiko mdomoni vikiwa na mayai,kukimbia kwa kuvaa magunia miguuni na kuvuta kamba.
Baadhi ya wanawake waliohudhuria maadhimisho ya siku ya mwanamke duniani wakishiriki mchezo wa kukimbia wakiwa wamevaa magunia miguuni.
Kila mwaka tarehe 8 mwezi Machi ni maadhimisho ya siku ya mwanamke duniani ambapo kwa mwaka huu 2019, kwa Wilaya ya Newala, maadhimisho hayo kiwilaya yamefanyika katika kata ya Kitangari na kauli mbiu ni "Badili fikra kufikia usawa wa kijinsia kwa maendeleo endelevu".
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa