Pichani ni Mkuu wa Wilaya ya Masasi Mhe. Selemani Mzee (wa katikati), Mkuu wa Wilaya ya Newala Mhe. Aziza Mangosongo, pamoja na viongozi wa vyama huru vya wafanyakazi Mkoa wa Mtwara wakiimba wimbo wa mshikamano wakati wa sherehe za Mei Mosi Mkoani Mtwara, zilizofanyika Kimkoa tarehe 1/5/2018 katika uwanja wa Sabasaba Wilayani Newala.
Wananchi wa Mkoa wa Mtwara na Tanzania kwa ujumla, wamehimizwa kuwekeza kwa wingi katika Mkoa wa Mtwara ili kuongeza tija ya maendeleo yao na ya Mkoa kwa ujumla.
Akitoa kauli hiyo wakati wa hotuba ya maadhimisho ya sikukuu ya wafanyakazi Duniani (Mei Mosi), iliyofanyika kimkoa tarehe 01/05/2018 katika uwanja wa sabasaba Wilayani Newala, Mkuu wa Wilaya ya Masasi Mhe.Selemani Mzee, ambaye ndio alikuwa mgeni rasmi katika sherehe hizo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, amesema suala la uwekezaji Mkoani Mtwara ni la muhimu sana, na ndio maana serikali kwa kuliona hilo, imetenga maeneo zaidi ya uwekezaji, yakiwemo ya Mtandi-Masasi, Mtwara Mikindani na eneo la msijute, yote haya yakiwa ni maalum kwa wawekezaji wanaotaka kuwekeza Mkoani Mtwara, hivyo wananchi wote wanakaribishwa kuwekeza Mkoani Mtwara.
Katika hotuba yake Mhe.Mzee amewaagiza waajiri wote wa sekta za umma na sekta binafsi, kuunda mabaraza ya wafanyakazi, ili yawe kiungo kati ya waajiri na watumishi wao, ikiwemo kuwarejesha kazini watumishi wote wa umma wa darasa la saba Mkoani Mtwara, walioondolewa kazini, kama serikali ilivyoagiza warejeshwe kazini mara moja.
Nao wafanyakazi wa Mkoa wa Mtwara katika risala yao ya wafanyakazi wa Mkoa wa Mtwara, iliyosomwa na Yusuph Stanford ambae ni Afisa Habari wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala, wameeleza suala la mishahara duni kwa wafanyakazi wa Tanzania, kiasi cha Tsh 100,000/= kwa mwezi, kinacholipwa katika sekta binafsi, hakikidhi mahitaji ya msingi ya binadamu, ukilingannisha na gharama halisi za maisha, na hivyo wameiomba serikali kupitia vyombo husika, kufanya mchakato wa kupitia upya viwango vya mishahara, na kuja na viwango vipya ambavyo vitaendana na hali halisi ya maisha ya sasa, ili kuboressha maisha ya mfanyakazi na kumpa hadhi katika jamii.
Aidha katika risala hiyo, wafanyakazi Mkoani Mtwara wameiomba serikali izingatie upandishwaji wa madaraja, ambao unaendana na urekebishaji wa mishahara ili kuleta hamasa kwa watumishi, kwani upandaji wa madaraja ni haki ya mtumishi, lakini kumekuwa na tatizo la watumishi kutopandishwa madaraja kwa wakati.
Hata hivyo wafanyakazi hao wameishukuru serikali ya awamu ya tano kwa kuanza kuitengeneza barabara ya kutoka Mtwara hadi Masasi kupitia Newala na Tandahimba km 50 kati ya km 210, ambayo kila mwaka ilikuwa ni kilio kikubwa katika risala ya wafanyakazi, na wameiomba serikali kuendelea kuitengea fedha barabara hiyo kwa km 160 zilizobaki kutoka Mnivata hadi Masasi, ili kuboresha usafiri wa watu na mizigo.
Pichani ni wafanyakazi wa Redio ya wananchi Newala (Newala Fm) (wa mbele kabisa) pamoja na wafanyakazi wa taasisi nyingine za Umma na serikali, wakiwa katika maandamano ya Mei Mosi Kimkoa Wilayani Newala.
Sherehe za MEI MOSI hufanyika kila tarehe moja ya mwezi wa tano kila mwaka, na kauli mbiu ya mwaka huu, ambayo ni tamko mahsusi la wafanyakazi kitaifa, ni “KUUNGANISHWA KWA MIFUKO YA HIFADHI YA JAMII, KULENGE KUBORESHA MASLAHI YA WAFANYAKAZI”
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa