Halmashauri ya Wilaya ya Newala imewarejesha kazini watendaji 56 wa vijiji ikiwa ni pamoja na kuwarejesha katika malipo yao ya mishahara kama ilivyo kawaida.
Akitoa taarifa ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala katika mkutano wa baraza la madiwani uliofanyika tarehe 7/8/2018 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Bwana Nsajigwa Sadick, amesema watendaji wa vijiji waliorejeshwa kazini ni wale waliotolewa kwa kukosa sifa ya Elimu ya kidato cha nne kutokana na maelekezo ya katibu mkuu Utumishi, na tayari wameshapangiwa vituo vya kazi,ambapo wanatakiwa waripoti katika vituo hivyo kabla ya tarehe 8/8/2018.
Wakati huo huo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Mhe.Chitwanga Rashid Ndembo amesema katika mwaka wa fedha wa 2017/2018, Halmshauri ya Wilaya ya Newala imetekeleza miradi kwa asilimia 40 tu kutokana na uwezo wa Halmashauri kupitia mapato ya ndani ambayo yaliathirika kutokana na ukosefu wa soko la mbaazi pamoja na ukosefu wa vyanzo vingine vya mapato ikiwa ni pamoja na serikali kupunguza tozo ya ushuru wa korosho au ushuru wa mazao ya biashara kutoka asilimia 5 hadi asilimia 3, kwani Halmashauri ilipanga bajeti yake kwa kuzingatia asilimia 5 ya ushuru wa korosho, hivyo kutokana na kupunguzwa kwa asilimia hizo kumepelekea kuathiri malengo ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Kufuatia hilo Halmashauri imejipanga vizuri kuhakikisha inakusanya mapato kwa wingi kupitia mashine za kukusanyia mapato ya halmashauri (POSS) ili kuweza kufanikisha malengo ya halmashauri ikiwa ni pamoja na kubuni vyanzo vingine mbalimbali vya mapato.
Katika hatua nyingine Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Newala, limefanya uchaguzi wa viongozi na wajumbe wa kamati za kudumu za Halmashauri ya Wilaya ya Newala, na kumchagua Makamu Mwenyekiti mpya wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Mhe.Rashidi Songoni wa CCM, aliyeshinda kwa kura 27 kati ya 29 dhidi ya mpinzani wake Mhe.Simon Nchingulu wa CUF, na kutangazwa na baraza kuwa ndiye Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri kuanzia tarehe 7/8/2018.
Mhe.Rashidi Songoni (wa mbele kabisa) Makamu Mwenyekiti Mpya wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala alipokuwa akiomba kura kwa wajumbe wa baraza mapema kabla ya uchaguzi wa makamu Mwenyekiti uliofanyika tarehe 7/8/2018 katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri ya Wilaya ya Newala.
Mhe.Songoni amechukua nafasi hiyo iliyokuwa inashikiliwa na Mhe.Swalehe Fakihi (CCM) kwa zaidi ya miaka miwili.
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa