Na Shabani Mkumba – Afisa Habari, Halmashauri ya Wilaya ya Newala
NEWALA, MTWARA – Julai 16, 2025
Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF) unaotekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Newala umeendelea kuleta mabadiliko chanya kwa wananchi kupitia afua mbalimbali zinazolenga kuinua maisha ya wananchi wa kipato cha chini.
Akitoa taarifa hiyo Julai 16,2025, Mratibu wa TASAF katika Halmashauri ya Wilaya ya Newala, Ndugu Benjamin Macha, amesema kuwa mpango huo unatekelezwa katika vijiji 107, ukihusisha kaya za walengwa 3,499 zenye wanufaika 10,536, wakiwemo wanawake 6,680 na wanaume 3,856.
Kwa mujibu wa Mratibu huyo, afua zinazotekelezwa kupitia TASAF ni pamoja na uhawilishaji wa fedha, utoaji wa ajira za muda (PWP), uundaji wa vikundi vya kuweka na kukuza uchumi, pamoja na utoaji wa ruzuku za uzalishaji kwa kaya zenye vigezo.
“Kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025, Halmashauri imepokea kiasi cha Shilingi 762,266,964.00 kwa ajili ya uhawilishaji wa fedha. Kati ya fedha hizo, Shilingi 607,822,056.00 ni kwa ajili ya malipo kwa kaya, na Shilingi 154,444,908.00 ni kwa ajili ya shughuli za usimamizi katika ngazi ya Halmashauri na vijiji,” amesema Macha.
Aidha, kupitia miradi ya ajira ya muda (PWP), Halmashauri imetekeleza miradi 116 yenye thamani ya Shilingi 308,050,424.48 kuanzia mwaka 2021 hadi 2025, ambapo walengwa wenye uwezo wa kufanya kazi walipewa ajira za muda huku wakishiriki katika miradi ya kijamii.
Kuhusu uundaji wa vikundi vya kuweka akiba, Ndugu Macha amefafanua kuwa hadi kufikia Juni 2025, Halmashauri imeunda jumla ya vikundi 324 vyenye wanachama 3,524 ambapo wanawake ni 2,725 na wanaume 799. Vikundi hivi vimefanikiwa kujiwekea akiba ya Shilingi 95,030,200.00 na kukopeshana Shilingi 43,681,600.00, ikiwa ni jitihada za kukuza uchumi wa kaya maskini.
Katika hatua nyingine, Halmashauri imewezesha kaya 75 kupokea ruzuku ya uzalishaji baada ya kutimiza vigezo. Kila kaya ilipata mtaji wa Shilingi 350,000.00, ambapo shughuli zilizofadhiliwa ni pamoja na uanzishaji wa biashara ndogondogo, ufugaji, ubanguaji wa korosho na ushonaji wa nguo.
Kwa mujibu wa Mratibu huyo, mafanikio makubwa yamepatikana kupitia utekelezaji wa mpango huo, ikiwa ni pamoja na watoto wote chini ya miaka mitano kuhudhuria kliniki kwa asilimia 100, na wanafunzi kutoka kaya za walengwa kuhudhuria shuleni kwa kiwango sawa.
Hata hivyo, amebainisha changamoto kadhaa zinazokabili utekelezaji wa mpango huo, zikiwemo baadhi ya walengwa kushindwa kuhudhuria siku za malipo, wasimamizi wa ngazi ya jamii (CMC) kujitoa, pamoja na baadhi ya vikundi kuvunjika.
“Tunayo mikakati ya kuimarisha utekelezaji wa mpango huu ikiwa ni pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa walengwa, kuimarisha usimamizi wa vikundi, na kuwasaidia kupata mikopo kupitia asilimia 10 ya mapato ya ndani ili kuongeza mitaji,” amesema Mratibu Benjamin Macha.
Kwa ujumla, mpango huu umeendelea kuboresha maisha ya wananchi na kuunga mkono juhudi za serikali katika kupunguza umasikini vijijini. Halmashauri ya Wilaya ya Newala inaendelea kusisitiza usimamizi na uwajibikaji katika kila ngazi ili kuhakikisha mafanikio haya yanaimarishwa zaidi.
Kitangari,Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa