Naibu waziri wa Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika, Mhe. Omary Mgumba alifanya ziara ya kikazi katika Wilaya ya Newala siku ya Jumamosi tarehe 26/01/2019.
Akiwa wilaya ya Newala Mhe. Mgumba alipata nafasi ya kupokea taarifa ya wilaya kutoka kwa mkuu wa Wilaya ya Newala Bi. Aziza Mangosongo, kuzungumza na wananchi wa Newala hasa wakulima kupitia mkutano mkuu uliofanyika katika kijiji cha Moneka na kupokea taarifa ya timu ya uhakiki wa wakulima wa korosho.
Akizungumza na wananchi wa Newala, Mhe. Mgumba alisema kuwa lengo la ziara yake ni kudumisha ukaribu wa Wizara yake na wadau wa sekta ya kilimo hasa wakulima, kufuatilia utekelezaji wa matamko ya Serikali, kuangalia maandalizi ya msimu mpya wa kilimo cha zao la korosho na mazao mengine, na kusikiliza changamoto za wananchi na kuzifanyia kazi.
Pia ziara hiyo ya Mhe. Mgumba ilikuwa na lengo la kufuatilia zoezi la uhakiki na malipo ya wakulima waliouza korosho na kutaka kujua sababu inayopelekea kuzidi kwa malalamiko ya wakulima wa korosho kuhusu malipo yao.
Akisoma taarifa ya Wilaya kwa Mhe. Mgumba, Mkuu wa Wilaya ya Newala Bi. Aziza Mangosongo alieleza kuwa Wilaya ya Newala ina jumla ya vyama vya msingi 55 na imekusanya jumla ya tani 41,489,536. Jumla ya wakulima 64,904 wametambuliwa na kwenye zoezi la uhakiki mpaka sasa jumla ya wakulima 58,569 wamehakikiwa kati ya hao wakulima 1653 ni wenye korosho zilizozidi kilo 1500 na wakulima 56,916 ni wenye korosho zilizo chini ya kilo 1500 na zoezi la uhakiki linaendelea.
Aidha mpaka sasa, kwa korosho zilizohakikiwa Serikali imekwishalipa jumla ya shilingi bilioni 47,479,836,864.85 kati ya bilioni 61 zinazotakiwa kulipwa.
Akizungumza na wananchi wa Newala, Mhe. Mgumba aliwaeleza kuwa malalamiko mengi yanasababishwa na mrejesho hafifu uliopo kati ya timu ya malipo na vyama vya msingi unaosababisha vyama vya msingi kutojua idadi na majina ya wakulima walikwisha kulipwa. Kutokana na hili Mhe. Mgumba ameagiza vyama vya msingi kupewa orodha ya majina ya wakulima waliolipwa na majina hayo yabandikwe kwenye ofisi za vyama hivyo vya msingi.
Pia Mhe. Mgumba ameeleza kuwa baadhi ya wakulima waliolipwa siyo waaminifu kwa kuwa wamepewa malipo yao ila wanadai kuwa hawajalipwa ili kukwepa majukumu mengine na kusababisha malalamiko kuwa mengi.
Akiendelea kueleza sababu za malalamiko kwa wakulima, Mhe. Mgumba amesema kuwa asilimia kubwa ya wakulima wana korosho daraja la pili ambalo halijalipwa mpaka sasa hivyo kuagiza wanaohusika na utoaji wa malipo hayo kuwalipa wakulima hao kwa kufuata kanuni na taratibu zinazoeleza korosho hizo za daraja la pili kulipwa kwa bei ambayo ni asilimia 80 ya 3,300 ambayo ni bei ya korosho daraja la kwanza.
Wakitoa maoni yao kwenye mkutano wa hadhara, wananchi wa Newala walimueleza Mhe.Mgumba kuwa kutokana na wakulima wa Newala kuvuna idadi nyingi ya korosho kiwango kilichowekwa na Serikali cha kilo 1500 kuwa ni kikubwa na kifanyiwe uhakiki kwa wakulima wa Newala ni kiwango kidogo sana hivyo kwa kipindi kingine waongeze idadi ya kilo zinazotakiwa kufanyiwa uhakiki. Pia walieleza kuwa mazao mengine ya kilimo msimu wake umeanza na utekelezaji wake unahitaji kipato ambacho wakulima wa Newala wanategemea kupata kutoka kwenye malipo ya zao la korosho hivyo kuchelewa kwa malipo hayo kunasababisha wakulima kushindwa kuendesha kilimo cha mazao mengine.
Mhe. Mgumba alowaondoa wasiwasi wakulima wa Wilaya ya Newala kwa kuwaahidi malipo yote ya wakulima wa korosho yatakamilika kufikia mwanzoni mwa mwezi wa pili mwaka huu.
Akikamilisha ziara hiyo, Mhe. Mgumba aliwashukuru wananchi wa Newala kwa mapokezi mazuri, aliipongeza Newala kwa kufanya uhakiki kwa wakati na kuwaeleza viongozi kuwa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Joseph Magufuli ametuteua kumsaidia kutatua shida za wananchi na wananchi wengi ni wakulima hivyo tusiogope kufanya maamuzi yaliyokuwa ndani ya uwezo wetu kwa mujibu wa miongozo, kanuni, sheria na kwa kuangalia maslahi ya umma.
Ziara ya Naibu waziri wa Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika kwa wilaya ya Newala ilikuwa ni ya siku moja na ilihudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Newala, kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya, uongozi wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Newala, timu ya uhakiki wa wakulima wa korosho, watumishi wa Serikali, wananchi wa Wilaya ya Newala na waandishi wa habari.
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa