Mkuu wa Wilaya ya Newala Mhe. Aziza Mangosongo, siku ya Jumatatu tarehe 04/11/2016 mbele ya wajumbe wa Halmashauri kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) aliwasilisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa Wilaya ya Newala katika kipindi cha miaka minne kuanzia 2016 hadi 2019 ikiwa ni utimizaji wa ahadi zilizotolewa kwenye Ilani ya CCM ya mwaka 2015-2020.
Mafanikio hayo yamewezeshwa na kutekelezwa na Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe. Rais John Pombe Joseph Magufuli ambapo kwa Wilaya ya Newala utekelezaji wa ilani umeonekana katika sekta za ujenzi, afya, elimu, barabara, maji, ardhi, maendeleo ya jamii na nishati.
Akiwasilisha utekelezaji huo, Mhe. Mangosongo ameeleza kuwa kwa Wilaya ya Newala mafanikio katika sekta ya afya yameonekana kwa kuongezeka kwa upatikanaji wa dawa kutoka 64% mwaka 2015 hadi 96% kwa mwaka 2019. Pia uboreshwaji wa utoaji wa huduma za afya ikiwa ni pamoja na ugawaji wa vyandarua vyenye viuatilifu hivyo kuzuia malaria, utambuzi wa wazee na ugawaji wa vitambulisho vya matibabu bure, ujenzi wa miundombinu ya zahanati na vituo vya afya, upatikanaji wa gari la kubebea wagonjwa, utoaji wa chanjo na upungufu wa hali ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI.
Mhe. Mangosongo pia aliwasilisha mafanikio ya sekta ya elimu kuwa kumekuwa na ongezeko la wanafunzi wanaojiunga na darasa la kwanza na kidato cha kwanza ambapo kwa darasa la kwanza uandikishaji mwaka 2016 ulikuwa ni kwa 86% na kwa mwaka 2019 ni 98%. Hii yote imetokana na Sera ya elimu bure iliyotolewa na Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe. Rais Magufuli. Katika sekta hii ya elimu pia ufaulu wa wanafunzi wa darasa la saba umeongezeka kutoka 56% mwaka 2016 hadi 98% mwaka 2019 na kidato cha nne kutoka 62.5% mwaka 2016 hadi 80.6% mwaka 2018. Mafanikio mengine ni pamoja na uimarishwaji wa usimamizi na ufuatiliaji kwa waratibu elimu kata kupatiwa pikipiki 39; ujenzi wa vyumba vya madarasa 69 na matundu 185 ya vyoo kwa shule za msingi na madarasa 55 na matundu ya vyoo 110 kwa shule za sekondari; ujenzi wa mabwalo 2 na mabweni 5.
Katika Wilaya ya Newala, utekelezaji wa ilani ya CCM ya mwaka 2015-2020 pia umeonekana kwenye ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka kilomita 8.67 mwaka 2016 hadi 12.97 mwaka 2019, ongezeko la upatikanaji wa maji safi na salama kutoka 38.7% mwaka 2016 hadi 61% kwa mwaka 2019; upimaji wa ardhi na utoaji wa hati 700 za umiliki wa ardhi na hati za kimila 183 na utengaji wa maeneo yenye ukubwa wa mita za mraba 269,300 kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda vidogo vidogo na vya kati.
Pia uwezeshaji wa vijana, walemavu na wanawake kwa kuwapatia mikopo yenye jumla ya shilingi 558,000,000.00 kwa vikundi 181; uhawilishaji fedha kwa kaya masikini 5179 na jumla ya shilingi bilioni tano zimetolewa na Serikali kwa ajili ya kunusuru kaya masikini kupitia TASAF; na upelekaji wa umeme vijijini kupitia mpango wa REA ambapo mpaka sasa jumla ya vijiji 33 vimepatiwa umeme na zoezi linaendelea.
Mhe. Mangosongo alieleza kuwa, Wilaya ya Newala imeendelea kutekeleza maagizo mbalimbali ya viongozi wakuu wa Serikali yakiwemo ufanyaji wa usafi kila jumamosi ya mwisho wa mwezi; ufanyaji wa mazoezi kupitia mabonanza mbalimbali yanayoandaliwa na Halmashauri husika; upigaji chapa kwa ng'ombe 1551; utoaji wa vitambulisho 9340 kwa wajasiriamali wadogo wadogo; na utumiaji wa mashine za kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato.
Pia upande wa Utawala bora kupitia Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe. Rais Magufuli, mapato ya ndani kwa Wilaya ya Newala yameongezeka kutoka bilioni mbili kwa mwaka wa fedha 2016/2017 hadi bilioni nne kwa mwaka 2018/2019 na Halmashauri za Wilaya ya Newala zimepata hati safi; ujenzi wa majengo ya Serikali yakiwemo jengo la utawala la Halmashauri ya mji wa Newala lenye ofisi 42, kumbi za mikutano na nyumba ya Mkurugenzi; ukarabati mkubwa wa nyumba ya Mkuu wa Wilaya ya Newala; ujenzi wa ofisi na nyumba za maafisa tarafa 2; ujenzi wa mahakama ya mwanzo ya Tarafa ya Mkunya; na ujenzi wa ofisi za kata na vijiji.
Wajumbe wa Halmashauri kuu ya CCM walipokea na kujadili mafanikio hayo na walipata nafasi ya kuwahoji watendaji wa Serikali katika sekta mbalimbali.
Kikao cha uwasilishaji wa utekelezaji wa ilani ya CCM ya mwaka 2015-2020 kiliongozwa na Katibu wa CCM Wilaya ya Newala Bw. Mussa Ramadhani Mwevi kwa niaba ya Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Newala na kilihudhuriwa na wajumbe wa halmashauri kuu ya CCM na watumishi wa Halmashauri ya Mji na Wilaya ya Newala.
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa