Kamati ya siasa ya Mkoa wa Mtwara ikiongozwa na mwenyekiti wa chama cha mapinduzi (CCM) Bw. Yusuph Said Nannila imefanya ziara ya kuona na kukagua utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi siku ya Jumapili tarehe 18/08/2019 katika maeneo ya Mkwedu, Kitangari na Mnyambe yaliyopo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Newala.
Akikagua majengo ya ofisi na nyumba ya afisa tarafa Mkwedu yaliyogharimu jumla ya shilingi milioni tisini, Bw. Nannila amewaeleza wananchi wa Mkwedu kuwa Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli itapeleka pia fedha shilingi milioni mia nne kwa ajili ya kuboresha majengo ya kituo cha afya cha Mkwedu na amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Bw. Mussa Chimae kutenga dirisha maalum la kuwahudumia wazee katika kituo hicho cha afya cha Mkwedu.
Kamati ya siasa Mkoa wa Mtwara ikipatiwa maelezo ya mradi wa chuo cha VETA Kitangari wakati wakikagua majengo ya chuo hicho.
Wakiendelea na ziara hiyo, kamati ya siasa ya mkoa pia ilikagua ukarabati wa majengo ya chuo cha VETA Kitangari ambapo Wizara ya Elimu, Sayansi na Tekinolojia kupitia VETA makao makuu imetoa fedha shilingi milioni mia mbili ishirini na mbili, laki tatu na elfu therathini na nne mia saba ishirini na moja kwa ajili ya kujenga vyoo vipya nane, ukarabati wa majengo ya kufundishia na utawala na ununuzi wa vifaa vya fani ya umeme, ushonaji na uhazili. Chuo hicho kinatarajiwa kufunguliwa rasmi mwezi Januari, 2020.
Bw. Nannila aliwaeleza wananchi kuwa ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ni ahadi ya chama kwa wananchi waliyoiweka wakati wa kampeni za kuomba kura ili wagombea wa chama cha mapinduzi waweze kuchaguliwa na wananchi. Hivyo ahadi zote zilizotajwa kipindi cha kampeni zinatakiwa kutekelezwa kama zilivyotolewa.
Ziara hiyo pia ilihusisha kukagua na kuona ujenzi wa bweni moja na madarasa mawili katika shule ya sekondari Mnyambe uliogharimu jumla ya shilingi milioni mia moja kumi na tano. Wanafunzi na walimu wa shule hiyo waliishukuru Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuendelea kuleta fedha za kuboresha miundombinu ya shule hiyo ambapo mpaka sasa wamepokea jumla ya shilingi milioni mia nne sabini na nne.
Ziara hiyo ya siku moja ilihusisha ukaguzi wa majengo kwa kulinganisha na thamani ya fedha iliyoletwa na Serikali. Majengo hayo ni pamoja na nyumba moja na ofisi ya afisa tarafa ya Mkwedu, ukarabati wa majengo chuo cha mafunzo ya ufundi stadi (VETA) Kitangari, bweni na madarasa katika shule ya sekondari Mnyambe.
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa