Baraza la madiwani la halmashauri ya Wilaya ya Newala, limewafukuza kazi watumishi 26 wa halmashauri ya Wilaya ya Newala baada ya kuthibitika na makosa mbalimbali ya kiutumishi.
Akithibitisha maamuzi hayo yaliyofanywa katika mkutano wa baraza la madiwani uliofanyika tarehe 29/04/2018 siku ya jumapili, mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Newala Mhe. Rashidi Chitwanga Ndembo amesema baraza limefanya maamuzi hayo baada ya kufanya uchunguzi wa kina na kufuata sheria na taratibu zote za kiutumishi, ambapo watumishi 14 kati yao, walibainika kuwa wameghushi vyeti vya kidato cha nne kwa miaka tofauti tofauti, na wengine 12 walifanya makosa ya utovu wa nidhamu ikiwa ni pamoja na kuidanganya halmashauri na serikali kwa ujumla, hivyo baraza la madiwani limeamua rasmi kuwafukuza kazi watumishi hao 26 wa halmashauri ya Wilaya ya Newala.
Katika hatua nyingine, kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Newala Mhandisi Nsajigwa P. Sadiki amewasilisha taarifa yake ambapo katika ukaguzi wa hesabu kwa mwaka wa fedha 2016/2017, halmashauri ya wilaya ya Newala imekuwa ni miongoni mwa halmashauri zilizopata HATI SAFI, jambo ambalo limetokana na jitihada na ushirikiano wa waheshimiwa madiwani na watendaji wake katika kuhakikisha halmashauri inafanya shughuli zake kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu.
Katika taarifa yake Mhandisi Nsajigwa ameongeza kuwa, kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018, halmashauri ya wilaya ya Newala imefanikiwa kununua gari mbili aina ya Toyota Hilux zenye thamani ya Tshs 179,917,273.90 ambapo kila gari limenunuliwa kwa Tshs 89,958,636.95, pamoja na pikipiki mbili kwaajili ya shughuli za uboreshaji wa ukusanyaji wa mapato na ugani.
Kupitia taarifa hiyo, Mkuu wa wilaya ya Newala Mhe. Aziza Mangosongo, ameipongeza halmashauri ya wilaya ya Newala kwa utendaji mzuri wa kazi na kupata hati safi, huku akisisitiza kuongeza jitihada zaidi katika swala la ukusanyaji wa mapato ya halmashauri.
Ikumbukwe kuwa serikali ya awamu ya tano imekuwa ikipambana vikali na watumishi walioghushi vyeti (vyeti feki), na wale wote wanaoshindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo, ikiwa ni pamoja na kuwashughulikia watumishi wanaokosa nidhamu ya kazi.
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa