Baraza la madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Newala leo tarehe 28/01/2021 limepitisha makadirio ya bajeti ya Tsh. 21,196,607,600 kwa ajili ya kugharamia matumizi mbalimbali ya Halmashauri na utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa mwaka wa fedha 2021/2022 kwenye mkutano uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa chuo cha walimu Kitangali.
Akiwasilisha rasimu ya bajeti hiyo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Bi. Magreth Likonda ameeleza kuwa makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti hiyo yanahusisha Tsh.11,800,007,100 kwa ajili ya mishahara toka Serikali kuu; Tsh. 12,021,000 kwa ajili ya mishahara itokanayo na mapato ya ndani ya Halmashauri; Tsh. 1,770,593,000 matumizi ya kawaida na Tsh.7,613,986,600 kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Aidha, wajumbe wa baraza la madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Newala baada ya kupokea uwasilishaji wa makadirio hayo ya bajeti walishauri kuwa ukusanyaji wa mapato ya ndani uongezeke ili kuwezesha kupeleka fedha nyingi zaidi katika miradi ya maendeleo hasa miradi ambayo imeanzishwa kwa nguvu ya wananchi na inahitaji msaada zaidi wa Halmashauri kwa ajili ya kukamilika.
Baraza hilo la madiwani lililofanyika maalum kwa ajili ya kujadili na kupitisha makadirio hayo ya bajeti limehudhuriwa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Newala Bw. Daniel Zenda aliyemwakilisha Mhe. Mkuu wa Wilaya ya Newala Aziza Mangosongo, wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Newala, waheshimiwa madiwani, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Bi. Magreth Likonda, wakuu wa idara na vitengo wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala, watumishi na waalikwa.
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa