Walimu wa shule za msingi katika Halmashauri ya Wilaya ya Newala leo Jumanne tarehe 04 Juni 2019 wametakiwa kutimiza wajibu wao ili kuwasaidia wanafunzi wanaowategemea kutimiza ndoto walizonazo.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Bw. Mussa Chimae wakati wa kikao kazi na walimu hao kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Bw. Mussa Chimae (aliyesimama) akisisitiza jambo wakati wa kikao kazi na walimu wa shule za msingi za Halmashauri ya Wilaya ya Newala.
Akizungumza kwenye kikao kazi hicho Bw. Chimae amewakumbusha walimu umuhimu na thamani yao katika maendeleo ya Halmashauri ya Wilaya ya Newala na nchi kwa ujumla. Amewataka walimu wafanye kazi kwa bidii ili ndoto za wanafunzi wanaowafundisha ziweze kutimia.
Kikao hicho kilihusisha kukumbushana maswala mbalimbali ya kiutumishi yakiwemo utekelezaji wa majukumu ya kila siku ya walimu katika maeneo yao ya kazi, upandishwaji wa madaraja kwa walimu, madai ya walimu, nidhamu pamoja na mishahara.
Wakiendelea na kikao hicho walimu walipata nafasi ya kutoa hoja mbalimbali walizonazo zikiwemo madai ya mishahara kwa walimu (arreas), upandishwaji wa madaraja kwa walimu waliojiriwa mwaka 2014, malipo ya uhamisho kwa walimu, kushuka kwa nidhamu ya wanafunzi kwenye baadhi ya shule za msingi na mchango wa mwajiri kwa walimu wanaotaka kujiendeleza kimasomo.
Afisa utumishi na utawala wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Bw. Famili Mshaghila akitolea ufafanuzi baadhi ya hoja za walimu kwenye kikao kazi cha walimu kilichoitishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala
Hoja hizo zilisikilizwa na kutolewa ufafanuzi na Afisa Utumishi na Utawala wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Bw. Famili Mshaghira na Afisa Elimu Msingi wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Bw. Ibrahim Mwakibete ambapo walimu walielezwa kuwa madai yao kama yalivyowasilishwa yamepokelewa na yanafanyiwa kazi, watumishi wanaotakiwa kupandishwa madaraja kwa sasa ni wale waliopo kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2017-2018 na waliotimiza miaka mitano kazini mpaka kufikia tarehe 30 June 2018 tangu kuajiriwa kwao.
Walimu wa shule ya msingi za Halmashauri ya Wilaya ya Newala wakisikiliza kwa makini kwenye kikao kazi kilichoitishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala.
Aidha Bw. Chimae pia amewataka watumishi kukaa kwenye vituo vyao vya kazi na wanapotaka kusafiri au wakiwa na udhuru wawe na ushahidi wa ruhusa zao kwa maandishi. Pia amewataka Waratibu Elimu Kata na Walimu Wakuu kuchukua hatua za kinidhamu pale inapobidi ili kuepuka mmomonyoko wa maadili katika maeneo yao ya kazi.
Kikao kazi hicho ni kikao cha kawaida ambacho Mkurugenzi Mtendaji hufanya na watumishi wake kwa makundi mbalimbali ambapo leo alifanya na walimu wote wa shule za msingi na kikao hicho kilihudhuriwa na Afisa Utumishi na Utawala, Afisa Elimu Msingi, Maafisa Elimu Kata, Walimu wakuu na walimu wote wa kawaida wa shule za msingi zilizopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Newala.
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa