Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu aipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Newala kwa kufanya vizuri katika viashiria vikuu vya Afya.
Akizungumza katika kikao maalumu na uongozi wa Wilaya, watumishi wa Halmashauri pamoja na viongozi wa vyama vya msingi vya ushirika Wilaya ya Newala, Mhe. Ummy Mwalimu alitoa pongezi hizo baada ya kusikia mafanikio hayo kutoka katika taarifa ya Wilaya iliyosomwa kwake na Mkuu wa Wilaya ya Newala Bi. Aziza Mangosongo.
Kwa mwaka 2018, kuanzia mwezi Januari, Halmashauri ya Wilaya ya Newala imetoa chanjo ya kujikinga na ugonjwa wa surua kwa asilimia 95, chanjo ya magonjwa ya watoto kwa asilimia 135, vifo vya mama wajawazito hakuna , vifo vya watoto wachanga 19 na vifo vya watoto chini ya miaka mitano vinne tu.
Mhe. Ummy Mwalimu, alieleza kuwa taarifa inaonyesha Halmashauri ya Wilaya ya Newala ina upungufu wa watumishi wa sekta ya Afya kwa asilimia 71 lakini hao wachache waliopo wanajitahidi kutekeleza majukumu yao ya kuwahudumia wananchi.
Pia, Mhe. Mwalimu aliahidi Serikali kuleta mashine mpya ya ‘x-ray’. katika hospitali ya Wilaya ya Newala ili kuongeza utoaji bora wa huduma za afya kwa wakazi wa Wilaya ya Newala
Ziara hiyo ya kikazi ya Mhe. Mwalimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Newala ilikuwa na lengo la kuangalia hali ya huduma ya afya katika eneo Halmashauri na kuhamasisha wananchi wa Newala ambao wengi ni wakulima kujiunga na fao la Ushirika Afya ambayo ni bima itakayowawezesha wakulima kutibiwa kwa mwaka mzima katika hospitali yoyote iliyopo ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ada ya Tsh. 76,800 tu kwa mtu mmoja
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa